Dodoma. Vilio simanzi na majonzi vimetawala nyumbani kwa aliyekuwa mchekeshaji na mshereheshaji wa shughuli mbalimbali nchini, marehemu Emmanuel Mathias (MC Pilipili) aliyefariki jana mchana jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu Mc Pilipili alikwenda jijini Dodoma kwa ajili ya kusherehesha harusi iliyokuwa ifanyike jana Jumapili Novemba 16,2025 lakini alikutwa na umauti na sababu za kifo chake bado hazijawekwa bayana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 17, 2025 nyumbani kwao Swaswa jijini Dodoma, dada wa marehemu, Veronica Mathias amesema alipata taarifa za kifo cha ghafla cha kaka yake baada ya kupigiwa simu na kaka yao mkubwa anayeishi Dar es salaam.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo alikwenda nyumbani kwao ili kujua kama taarifa hizo ni kweli na alipofika alikuta taarifa hizo ni za kweli.
”Kwa kweli sijui ni nini kimempata kaka yangu mpaka kifo kikamkuta, imekuwa ni ghafla mno kuna ndugu yetu mmoja aliyeuona mwili wake amesema ulikuwa na madoa meusi mgongoni yanayoonekana kuwa ni majeraha,” amesema Veronica.
Amesema mpaka sasa hawajui maziko yatakuwa lini kwani bado wanamsubiri kaka yao mkubwa kutoka Dar es salaam, kwa ajili ya kupanga siku ya mazishi.
Kuhusu mke wa marehemu na mtoto kuhudhuria msibani, Veronica amesema hawana mawasiliano nao na mpaka sasa bado hawajafika Dodoma msibani.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya maafa Mtaa wa Swaswa, Pascal Maingu amesema kifo cha MC Pilipili kimeshtua wakazi wa mtaa huo kutokana na maisha waliyokuwa wanaishi na mshereheshaji huyo.
”Alikuwa ni kijana mzuri mchangamfu na mwenye upendo kwa majirani zake, alikuwa akifika hapa ni lazima apite nyumba kwa nyumba kuwasalimia na kuwachekesha kama ilivyokuwa kawaida yake,” amesema Maingu.
Amesema utaratibu wa mazishi unasubiri vikao vya ndugu ambapo mwili bado upo chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Mtumba ambaye pia alikuwa rafiki wa karibu na MC Pilipili, Anthony Mavunde amesema Mc Pilipili alikuwa ni mmoja wa vijana wa Mkoa wa Dodoma ambao waliutangaza vema mkoa kwa kupitia tasnia ya ushereheshaji pamoja na uchekeshaji ambapo alijizolea umaarufu mkubwa.
Amesema MC Pilipili alikuwa ni mtu wake wa karibu pamoja na wasanii wengine wa mkoa huo akiwamo mwanamuziki Ben Paul ambao wamekuwa wakimchukulia kama kaka na wamekuwa wakikaa pamoja kama ndugu kwa kushiriki shughuli nyingi zikiwemo matukio mengi ya kijamii na kisiasa.
“Kwa kweli msiba huu umenigusa sana kwa sababu umekuwa ni ghafla na niliwasiliana naye leo (jana) asubuhi akanijulisha anakuja Dodoma ana kazi ya UMC (kusherehesha), na akaniomba akimaliza anatamani kuzungumza na mimi na bahati mbaya tumeshindwa kuonana mauti yamemfika, lakini nimeshtushwa na kifo cha Emmanuel,” amesema Mavunde.
Mmoja wa marafiki za MC Pilipili ambaye walisoma wote Shule ya Msingi Ipagala, Frank Mamba amesema kuwa alipata taarifa za msiba baada ya kupigiwa simu na wenzake waliosoma nao.
Amesema awali alizipuuza habari hizo kwani haikuwa mara ya kwanza kwa MC huyo kuzushiwa kifo, hata baada ya uchaguzi mkuu walizusha kuwa amefariki dunia.
”Kati ya Oktoba 30 na 31 nilipokea simu ikiniuliza kama nina taarifa za kifo cha MC Pilipili nilichukua hatua ya kumpigia simu alipokea na nikaongea naye na kunihakikishia kuwa ni mzima wa afya na anaendelea na shughuli zake, hii taarifa ya sasa pia niliipuuza lakini nilipopiga simu zake zilikuwa hazipatikani na siyo kawaida yake,” amesema Mamba.
Amesema haikuwa kawaida kwa MC Pilipili kuzima simu zake muda wote na hivyo kitendo cha kutopatikana jana kilimthibitishia kuwa ni kweli amefariki.
Mamba amesema alilazimika kwenda chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambapo alithibitisha ni kweli MC huyo amefariki.
Nabii Richard Magenge, aliyekuwa msimamizi wa harusi ya MC Pilipili, amesema ameondokewa na kijana aliyekuwa na heshima, upendo na uaminifu mkubwa katika kazi na mahusiano ya kila siku.
Akizungumza jana, Magenge alisema alimfahamu kwa ukaribu kupitia kazi za sanaa na shughuli mbalimbali za kijamii, akimtaja marehemu kama msanii mwenye maono makubwa na mwenye moyo wa kusaidia watu.
Alieleza kuwa MC Pilipili alikuwa amerejea jijini Dodoma kuendeleza kazi zake za sanaa pamoja na mikakati mingine aliyokuwa ameipanga.
Hata hivyo, Magenge alisema siku ambayo familia ilikuwa imepanga kufanya kikao maalum, ndiyo siku ambayo msanii huyo alipoteza maisha, Novemba 16. Alisema tukio hilo limeiacha familia na watu wa karibu katika majonzi makubwa, kwani walikuwa wakitarajia kukutana kwa mazungumzo muhimu ya kifamilia.
Msanii wa filamu nchini, Steven Mengele maarufu kama Steve Nyerere, amesimulia namna alivyomfahamu kwa ukaribu marehemu MC Pilipili, aliyefariki dunia Novemba 16, 2025, mkoani Dodoma.
Akimzungumzia marehemu, Steve Nyerere amesema kuwa MC Pilipili alikuwa mtu mwenye moyo wa upekee, aliyependa kuwaunga mkono wenzake na kuwafanya wengine watabasamu hata katika nyakati ngumu. Ameeleza kuwa urafiki wao ulijengwa kwa muda mrefu kupitia kazi za sanaa, ambapo alimfahamu MC Pilipili kama msanii mwenye nidhamu, ubunifu mkubwa na anayeheshimu watu wote.
Steve Nyerere pia ametuma salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na wadau wote wa tasnia ya burudani, akibainisha kuwa sekta ya sanaa imepoteza kijana mwenye kipaji kikubwa na mchango mkubwa katika kukuza sanaa ya vichekesho nchini.
Kutokana na utata wa kifo cha MC Pilipili, Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera kujua nini kimesababisha kifo cha msanii huyo.
Kamanda Hyera alijibu kwa kufupi kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu kifo cha ghafla cha MC huyo na watatoa taarifa baadaye uchunguzi utakapokamilika.
