WAKATI kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara akitarajiwa kufanyiwa upasuaji kesho Jumanne Novemba 18, 2025 huko Morocco, beki wa kati Abdulrazack Mohamed Hamza naye ametajwa kuwa mbioni kwenda nchini humo kwa ajili ya matibabu ya goti.
Camara ambaye huu ni msimu wake wa pili akiwa na wekundu hao wa Msimbazi, aliondoka nchini jana Jumapili Novemba 16, 2025 kwa ajili ya kwenda Morocco kwa ajili ya upasuaji wa goti ambalo litamfanya kukaa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi 10.
Akizungumza kuhusu hali ya kikosi hicho ambacho kinajiandaa na mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kinachoendelea kwa wachezaji hao.
Ally amesema hao ndio wachezaji pekee kwa mujibu wa ripoti ya meneja Dimitar Pantev ambao watakosekana katika mechi hiyo ambayo itachezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Hamza bado anaendelea na matibabu, wiki hii ataenda Morocco kwa ajili ya uangalizi,” amesema huku akigusia kuhusu urejeo wa Mohammed Bajaber ambaye alikuwa majeruhi tangu wakati wa maandalizi ya msimu huu.
Amesema kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Kenya amerejea na alipata nafasi ya kucheza katika mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania wakati wakiishindilia mabao 6-0.
“Amerudi na meneja alimpa dakika za kucheza, hivyo amerudi,” ameeleza.
Alipotoa kauli hiyo, shangwe liliibuka kwenye soko la Sterio, Temeke ambapo Simba ilikuwa ikitangaza viingilio na kuweka wazi ratiba yake ya hamasa kwa lengo la kuujaza Uwanja wa Benjamini Mkapa katika mechi hiyo.
“Uzinduzi wa hamasa utakuwa Jumatano Novemba 19, 2025 na kwa mara ya kwanza utafanyika Chanika Zingiziwa. Msafara wetu utaanzia Buguruni, Ukonga, Pugu, Chanika tunamaliza yote na tutakwenda kufanya balaa huko,” amesema na kuongeza;
“Nichukue nafasi hii kuwakaribisha Wanasimba wote twende Zingiziwa kwenye uzinduzi wa hamasa.”
Kwa upande wa viingilio katika mechi hiyo, Ally amesema kwa Tanzanite ni Sh250,000, Platnumz Sh150,000, VIP A Sh30,000, VIP B Sh20,000, VIP C Sh10,000 huku mzunguko ikiwa ni Sh5,000.
Ally pia ameeleza kuhusu uzinduzi wa jezi mpya za kimataifa kwa kusema zitazinduliwa Alhamisi ya Novemba 20, 2025 na kuwaambia Wanasimba wawe tayari kwa mtoko huo.
