Jumuiya ya Madola kusaka maridhiano Tanzania

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikisaka njia ya maridhiano, Jumuiya ya Madola imemteua Rais mstaafu wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo nchini kuunga mkono majadiliano ya maridhiano na maendeleo.

Hatua hiyo, inamfanya Dk Chakwera kuongoza ujumbe wa jumuiya hiyo kwa kufanya ziara ya siku nne nchini kuanzia kesho Novemba 18, kufanya majadiliano kuhusu uchaguzi na mchakato mpana wa maridhiano.

Hayo yote yanakuja, katikati ya juhudi za Serikali kufanya maridhiano, baada ya kutokea kwa maandamano yaliyosababisha vurugu siku ya uchaguzi Oktoba 29 na 30 mwaka huu.

Kutokana na vurugu hizo, watu kadhaa walipoteza maisha, baadhi waliharibiwa mali, biashara na miundombinu ya umma ilichomwa moto na waandamanaji.

Kama juhudi za kuutafuta mwafaka, Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 14, mwaka huu katika hotuba yake bungeni, alitangaza kuhuzunishwa na vifo vilivyotokea, huku akiomba msamaha na kuachiwa huru kwa waliokamatwa kwa tukio hilo.

Ameambatanisha salamu zake hizo za rambirambi na wito wa wadau mbalimbali na makundi mengine kuunga mkono juhudi za maridhiano ili kupatikana mwafaka kwa masilahi ya nchi.

Taarifa ya Jumuiya ya Madola

Katika taarifa yake ya leo, Jumatatu, Novemba 17, 2025, iliyochapishwa kwenye tovuti ya Jumuiya ya Madola, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Shirley Botchwey, amemteua Dk Chakwera kuongoza ujumbe wa majadiliano hayo na wadau mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya sekretarieti ya jumuiya hiyo, Dk Chakwera anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya siku nne, kuanzia Novemba 18 hadi 21 na ataanzisha majadiliano jumuishi na wadau wa Tanzania kuhusu masuala yanayohusiana na uchaguzi na mchakato mpana wa maridhiano.

Katika kipindi cha ziara hiyo, Dk Chakwera atakutana na viongozi wa Serikali, viongozi wa vyama vya siasa, wawakilishi wa asasi za kiraia, viongozi wa dini na mila, pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi.

Uteuzi huo unafuatia kauli ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu Botchwey kuhusu hali ya kisiasa nchini na dhamira yake ya kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuimarisha majadiliano ya kitaifa.

“Uzoefu na uongozi wa Dk Lazarus Chakwera utakuwa muhimu katika kusaidia majadiliano ya kujenga kati ya wadau wote. Ninaamini utasaidia kuleta amani na utulivu kwa watu wa Tanzania kulingana na misingi ya Jumuiya ya Madola ya ujumuishi, haki na uwajibikaji,” amesema.

Kwa upande wake, Dk Chakwera alikubali uteuzi huo kwa heshima.

“Kama Mwafrika kutoka nchi jirani ambaye amefuatilia kwa karibu hali ya Tanzania, nina heshima kubwa kuteuliwa kuwa mjumbe maalumu. Nimejitolea kikamilifu kusaidia majadiliano jumuishi yanayolinda misingi ya kidemokrasia na kuimarisha utawala wa sheria,” amesema Dk Chakwera.

Dk Chakwera ataungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Profesa Luis Franceschi, huku matokeo ya ziara hiyo yakitarajiwa kuiongoza Jumuiya ya Madola katika uamuzi na hatua zinazofuata kupitia Good Office za Katibu Mkuu.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema bado hana taarifa kuhusu hilo. “Ndio kwanza nakusikia wewe, nipo safarini.”

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Jumuiya ya Madola kutuma ujumbe wake kwa lengo la majadiliano na kutafuta maridhiano.

Tofauti yake ilitokea mwaka 1995, wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Chifu Emeka Anyaoku, alimteuwa Dk Moses Anafu kusimamia mazungumzo ya maridhiano katika mgogoro kati ya Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

Mzizi wa mgogoro ulikuwa masuala ya uchaguzi na juhudi hizo ndizo zilizozaa makubaliano yaliyoitwa Mwafaka wa kwanza wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Mwafaka huo ulipendekeza kufanyika kwa marekebisho ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), marekebisho ya Katiba ya Zanzibar na makubaliano kufidiwa kwa walioathirika kutokana na vurugu.

Kutokana na hilo, wawakilishi wawili wa CUF waliteuliwa kuwa wajumbe wa baraza la wawakilishi na kuanzishwa kwa kamati kutoka ndani ya vyama kusimamia utekelezaji.