KOCHA wa AS Maniema Union, Papy Okitankoyi Kimoto, ni kama ameitumia salamu Azam FC kimtindo baada ya kusema wanataka kuanza kampeni ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwa ushindi, huku malengo yao makubwa ni kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu na kufuzu robo fainali.
Kauli ya Kimoto imekuja wakati huu ambao AS Maniema inajiandaa kuikaribisha Azam katika mechi ya kwanza ya Kundi B la michuano hiyo itakayochezwa Stade des Martyrs, Kinshasa nchini DR Congo, Novemba 23, 2025.
Azam imefuzu makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza tangu kuanza kushiriki mwaka 2013 ambapo imepangwa Kundi B na timu za AS Maniema ya DR Congo, Wydad Athletic (Morocco) na Nairobi United (Kenya).
Kwa upande wa AS Maniema, imekuwa ikicheza makundi mara kwa mara na msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika, iliburuza mkia wa Kundi B kwa kukusanya pointi tatu. Kundi hilo liliongozwa na AS FAR Rabat iliyomaliza na pointi 10, ikifuatiwa na Mamelodi Sundowns (pointi 9), ya tatu Raja Club Athletic (pointi 8).
Akizungumzia mechi hiyo na kundi walilopo kwa ujumla, Kimoto amesisitiza kumuheshimu kila mpinzani wao, huku akieleza kuwa Maniema wanataka kuanza vizuri nyumbani kabla ya safari ndefu kwenda Morocco, Tanzania na Kenya.
“Tunaanzia nyumbani ambako tunataka kuwa na mwanzo mzuri kwani malengo yetu yako wazi, ni kucheza robo fainali msimu huu.
“Msimu uliopita tulikosa hiyo nafasi, uzoefu huo umetufundisha mengi na utatusaidia kuimudu hatua hii ya makundi vizuri zaidi.
“Furaha niliyonayo ni kwamba tunawafahamu wapinzani wetu. Hizi ni timu zenye vipaji, kila moja imepata nafasi kwa kustahili kama sisi.
“Mechi ya kwanza tunacheza na Azam ambao licha ya ushiriki wao wa kwanza hatua hii, lakini wamejiandaa vizuri sana mwaka huu. pia kuna Nairobi, waliowatoa vigogo wa Tunisia, Etoile du Sahel. Timu hizi hazipaswi kupuuzwa,” amesema kocha huyo.
Hata hivyo, katika kundi hilo, Wydad ambao ni washindi mara tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wanatajwa kuwa ndiyo timu tishio zaidi huku Kimoto raia wa DR Congo akisema: “Tutakutana na gwiji wa Afrika, Wydad Athletic Club ya Casablanca, timu tunayoiheshimu sana, hivyo lazima tujipange kisawasawa kucheza na wapinzani wote ili kufikia malengo.”
