Maswa yajipanga kuokoa watoto njiti, yasambaza vifaa tiba

Maswa. Hospitali ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeendelea kuboresha huduma kwa watoto njiti na wenye uzito pungufu, kwa kusambaza mashine maalumu za kuwahudumia watoto wachanga katika vituo kadhaa vya afya.

 Lengo ni  kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi.

Vifaa vilivyosambazwa vinajumuisha mashine za kurekebisha joto la mwili wa mtoto mchanga pamoja na mashine za kutibu manjano. Vituo vya afya vilivyonufaika ni Malampaka, Lalago, Mwabayanda, pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Maswa.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Hadija Zegega(kulia)akimkabidhi mashine moja kwa ajili ya watoto Njiti,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Maswa,Dk Deogratius Mtaki.Picha na Samwel Mwanga

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa hospitali hiyo kuboresha huduma za afya za mama na mtoto, hususan katika maeneo ya vijijini ambako wazazi wengi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda.

Akizungumzia mpango huo, leo Jumatatu, Novemba 17, 2025 wakati wa kuadhimisha siku ya watoto njiti, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Hadija Zegega amesema kusambazwa kwa mashine hizo kutaiwezesha wilaya hiyo kutibu na kutunza watoto njiti bila kulazimika kuwapeleka hospitali za rufaa.

“Tumegawa mashine hizi ili huduma ziwafikie wananchi kwa haraka. Awali, wazazi walipata taabu kusafirisha watoto njiti hadi katika hospitali zilizo mbali, jambo ambalo liliongeza hatari ya vifo. Hii ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ya watoto wengi,” amesema.

Hii ni moja ya mashine ya kuwahudumia watoto Njiti ambapo vituo vya Afya vya Lalago,Malampaka na Mwabayanda kila kimoja kimepata mashine moja.Picha na Samwel Mwanga

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto katika hospitali hiyo, Sakina Mkwende amesema ongezeko la watoto wanaozaliwa njiti limeifanya hospitali kuongeza nguvu kwenye huduma hizo ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa kupatiwa tiba.

Amesema kwa mwaka 2024, walihudumia watoto 97 waliokuwa njiti na wenye uzito pungufu, lakini walikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo.

“Takwimu zinaonyesha idadi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu inaongezeka. Kwa kupata na kusambaza vifaa hivi, tuna hakika huduma zitakuwa bora na salama zaidi kwa watoto wachanga. Kwa mwezi tunapokea watoto kati ya 45 hadi 60 wenye mahitaji maalumu,” amesema.

Mganga mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Hadija Zegega(kulia)akimkabidhi,Joseph John(kushoto)ambaye ni Mfamasia wa wilaya hiyo kifaa cha kupimia watoto njiti.Picha na Samwel Mwanga

Baadhi ya wananchi wamesema hatua hiyo imekuja wakati mwafaka huku wakieleza kuwa itaondoa gharama na usumbufu wa kusafirisha watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando iliyoko jijini Mwanza.

Neema John, mkazi wa Kijiji cha Lalago, wilayani Maswa, amesema walikuwa wakitumia gharama kubwa kwenda kupata huduma hiyo katika hospitali ya rufaa ya Bugando iliyopo mjini Mwanza.

“Tulikuwa tukipata shida sana kusafiri na watoto wadogo kwenda Bugando kwa matibabu ya uzito pungufu. Sasa huduma zipo karibu, ni faraja kubwa kwa familia,” amesema.

Naye Juma Paul, mkazi wa Malampaka, amesema ni hatua ya kupongezwa kwa Serikali kufanya uwekezaji wa aina hiyo ambao utasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga.