Mawasiliano nyenzo muhimu kufikia matumizi nishati safi ifikapo 2034

Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wanne kati ya watano ifikapo mwaka 2034 ukiendelea imeelezwa mawasiliano ni dira muhimu kufanikisha lengo hilo.

Imeelezwa mkakati wa mawasiliano wa nishati safi ya kupikia ni dira muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi na salama, rafiki wa mazingira na yenye gharama nafuu ifikapo  mwaka 2034 ambapo asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 17, 2025 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Neema Mbuja wakati akizungumza na wananchi katika kipindi cha Crown Sport Jijini Dar es Salaam.

Neema amesema mkakati wa nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu katika kutekeleza makubaliano ya kitaifa na kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kupunguza uzalishaji wa gesi joto.  

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Neema Mbuja

“Kupitia Mkakati wa Taifa wa miaka kumi, Serikali inalenga kufikisha asilimia 80 ya kaya za Tanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Mkakati huu unajikita katika kupunguza magonjwa ya kupumua yanayotokana na moshi, kulinda misitu.

“Aidha kuongeza fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji katika teknolojia na vifaa safi vya kupikia pia Serikali imesisitiza kuwa utekelezaji wa mkakati huo utahusisha sekta binafsi, taasisi za maendeleo, na jamii kwa ujumla zinazolisha watu zaidi ya 100 kama Shule na Magereza,” ameeleza.

Amesema, mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia unakwenda sambamba na mkakati wa mawasiliano kwani umelenga kuamsha uelewa wa Watanzania kupata taarifa juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema kupitia kampeni za kitaifa zitakazohusisha redio, televisheni, mitandao ya kijamii, maonyesho ya wazi, pamoja na mafunzo maalum kwa viongozi wa jamii, waandishi wa habari na washawishi wa mitandaoni  Watanzania wanapata ujumbe mahususi na uelewa  kuhusu nishati safi ya kupikia.

Mhandisi wa Utafiti Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Samwel Kessy

Kwa upande wake, Mhandisi wa Utafiti Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Samwel Kessy ameeleza mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia ni dhana muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati  safi ya kupikia, kuokoa muda, pamoja na kupunguza gharama za matumizi, athari za kimazingira na kiafya kwa watumiaji.

 “Sisi kama Tanesco tumehakikisha umeme umewafikia wateja kwa kiasi kikubwa na unapatikana kwa haraka lakini pia kwa kushirikiana na sekta binafsi tumehakikisha wananchi wanapata vifaa bora vya kupikia na vyenye gharama nafuu, ili waweze kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesisitiza.