Mshangao mabadiliko Baraza la Mawaziri

Dar es Salaam. Ni mshangao. Ndivyo unavyoweza kulielezea baraza jipya la mawaziri ambalo Rais Samia Suluhu Hassan amelitangaza, likiwa na sura mpya, huku baadhi ya waliokuwa kwenye baraza lililopita wakirejea na wengine wakitemwa.

Rais Samia ameteua baraza hilo leo Novemba 17, 2025, likiwa na mawaziri 27, huku akiunda wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana, itakayokuwa katika Ofisi ya Rais, lengo likiwa ni kushughulikia masuala ya vijana.

Vilevile, Rais Samia ameirudisha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoka Ofisi ya Rais kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, kama ilivyokuwa zamani, lengo likiwa ni kumpa nafasi Waziri Mkuu kusimamia shughuli za kila siku za Serikali.

Pia, Rais Samia amesema wamefanya mabadiliko kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Uhusiano kwa kuiondoa Vijana ambayo imekuwa wizara kamili. Amesema Waziri wa wizara hiyo atakuwa na jukumu la kuimarisha uhusiano kwa kukutana na makundi tofauti ili kujenga uhusiano mzuri.

Baraza hilo la kwanza katika kipindi chake cha pili, limechukua sura mpya za watu ambao wamefanya kazi katika maeneo tofauti, ikiwamo wakuu wa mikoa, makatibu wakuu wastaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na makatibu wakuu wa zamani.

Katika uteuzi huo, Rais Samia amewateua mawaziri wapya wanane ambao hawakuwahi kuwa mawaziri kabla, jambo ambalo linaonesha imani kubwa aliyonayo kwao katika wizara alizowateua ili wakamsaidie kazi.

Miongoni mwa mawaziri hao ni makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Daniel Chongolo ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Dk Bashiru Ally aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Vilevile, amemteua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na mtaalamu wa uchumi, Joel Nanauka ambaye ameteuliwa kwenye Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.

Rais Samia amemteua Balozi Khamis Mussa Omar, aliyemteua kuwa mbunge Novemba 10, kuwa Waziri wa Fedha, akichukua nafasi ya Dk Mwigulu Nchemba aliyeteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.

Wengine walioteuliwa ni Rhimo Nyansaho, aliyeteuliwa na Rais Samia kuwa mbunge, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, wizara ambayo katika baraza lililopita iliongozwa na Dk Stergomena Tax.

Katika Wizara ya Tamisemi, Rais Samia amemteua Profesa Riziki Shemdoe kuwa Waziri. Profesa Shemdoe alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kabla ya kujitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Lushoto na kushinda.

Dk Leonard Akwilapo, aliyekuwa Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali serikalini kabla ya kugombea ubunge katika Jimbo la Masasi, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi.

Kwenye uteuzi huo, Rais Samia amemteua Mbunge wa Rufiji Omary Mchengerwa kuwa Waziri wa Afya akichukua nafasi ya Jenista Mhagama, aliyeongoza wizara hiyo katika awamu iliyopita.

Kwa upande wa manaibu waziri wapya, Rais Samia amewateua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Dk Ngwaru Maghembe na James Ole Millya kuwa manaibu waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika Wizara ya Fedha, amewateua manaibu wawili wapya ambao ni Laurent Luswetula na Mshamu Ali Munde. Pia, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Uhusiano, amemteua Rahma Riadh Kisuo kuwa Naibu Waziri.

Manaibu waziri wengine wapya ni Regina Qwaray (Utumishi wa Umma), Pius Chaya (Mipango na Uwekezaji), Reuben Kwagilwa na Dk Jafar Rajab Seif (Tamisemi), Switbert Mkama (Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), na Wanu Hafidh Ameir (Elimu, Sayansi na Teknolojia).

Wengine ni Dk Ng’wasi Kamani (Mifugo na Uvuvi), Salome Makamba (Nishati), Paul Makonda (Habari, Utamaduni na Michezo), Kaspar Mmuya (Ardhi, Nyumba na Makazi), na Dk Florence Samizi (Afya).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa, amesema sura mpya katika Baraza la Mawaziri si jambo la kushangaza, kwani dalili za mabadiliko hayo zilianza kuonekana tangu baadhi ya viongozi wa muda mrefu walipoacha nyadhifa zao.

Profesa Kahangwa amesema hatua ya waliokuwa wakuu wa mikoa kama Paul Makonda, Chongolo na Dk Homera kuachia ngazi ilikuwa ni ishara ya maandalizi ya safari ya kuingia katika ngazi za juu za uongozi.

“Kwa mfano, Dk Bashiru alikuja kuteuliwa ubunge. Haya yote yalionesha wazi kuwa kulikuwa na mpangilio wa mabadiliko mapema,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Kahangwa, uteuzi huo umeleta sura mpya huku baadhi ya viongozi wenye uzoefu wakiachwa pembeni, jambo alilosema linaweza kuashiria kwamba Rais anawafahamu vema walioteuliwa na ameridhishwa na utendaji wao wa awali.

“Baraza la Mawaziri mara nyingi huakisi matendo ya kisiasa ndani ya chama na mikondo ya kampeni. Inawezekana hawa wapya walikuwa na mchango mkubwa kwa namna moja au nyingine,” amesema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulkarim Atiki amesema uteuzi huo umeibua mshangao kwa watu waliodhani wanaweza kutabiri mwelekeo wa Rais.

“Safari hii wameachwa midomo wazi. Walitarajia majina fulani, lakini matokeo yamekuwa tofauti,” amesema.

Atiki ameongeza kwamba kwa kawaida asilimia 70 ya baraza huwa ni watu wazoefu na asilimia 30 wapya, lakini safari hii uwiano huo umegeuzwa, ishara kwamba Rais amedhamiria kuleta mtazamo mpya.

Amesema ujio wa vijana kama Nanauka ni hatua muhimu, kwani Tanzania ina idadi kubwa ya vijana ambao kwa muda mrefu walikosa uwakilishi wa karibu.

“Nanauka anajua nguvu, mahitaji na fikra za vijana. Ni jambo jema kuona mwakilishi wa kizazi kipya akipewa nafasi ya kufanya maamuzi ya kitaifa,” amesema.

Naye Balozi Benson Bana amesema uteuzi huo unaonesha Rais Samia ana imani na timu aliyoiunda katika kuhakikisha ilani ya chama inatekelezwa ipasavyo.

“Ni mchanganyiko mzuri wa wakongwe na vijana. Tuipe muda. Ni mapema kuanza kuhoji utendaji wao, au kutabiri watafanya mambo gani kukidhi matarajio ya wananchi,” amesema.

Kwenye baraza hilo, wapo mawaziri waliorejea katika kipindi cha pili cha Serikali ya awamu ya sita, huku baadhi wakibadilishwa wizara na wengine wakibakishwa katika wizara za awali.

Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, amebakishwa katika wizara aliyokuwapo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.

Mwingine aliyebakishwa katika wizara ni Hamad Masauni akiwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, na naibu wake ni Dk Festo Dugange.

Katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, ameteuliwa tena katika wizara hiyo, huku naibu wake akiwa ni Ummy Nderiananga.

Vilevile, Balozi Mahmoud Thabit Kombo naye ameendelea kushika wadhifa wake katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mwingine anayeendelea katika wizara ya zamani ni Profesa Adolf Mkenda aliteteuliwa tema kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Katika Wizara ya Maji, Jumaa Aweso ameendelea na wadhifa huo, na naibu wake ni Kundo Mathew. Profesa Palamagamba Kabudi anaendelea kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, na naibu mawaziri wake ni Hamis Mwinjuma na Makonda.

Anthony Mavunde amebakishwa kuwa Waziri katika Wizara ya Madini, na naibu wake ni Dk Steven Kiruswa, huku Dk Ashatu Kijaji akiteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na naibu wake ni Hamad Hassan Chande.

Waliobadilishwa wizara ni pamoja na George Simbachawene, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na naibu wake ni Dennis Londo. Vilevile, Profesa Makame Mbarawa ataendelea kuwa Waziri wa Uchukuzi, na naibu wake ni David Kihenzile.

Kadhalika, Deogratius Ndejembi ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati, na naibu wake akiwa ni Salome Makamba ambaye ni mmoja wa waliokuwa wabunge 19 wa Viti Maalumu-Chadema, kabla hajatimkia CCM.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na naibu wake ni Regina Qwaray.

‘Wenye sifa ni wengi’

Akizungumzia uteuzi huo, mchambuzi wa siasa Magabilo Masambu amesema ongezeko la sura mpya katika Baraza la Mawaziri ni kiashirio kwamba wenye sifa ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo ni wengi, na waliobaki kwenye baraza hilo wameaminiwa kwa uwezo wao.

“Rais anataka kuonesha mabadiliko kwamba uongozi ni mpya. Sasa wapo mawaziri ambao wametoka kuanzia awamu ya tano na bado wapo kwenye nafasi zao, maana yake wanafanya vizuri na wangefanya vibaya wangeondolewa muda mrefu,” amesema.

Mchambuzi mwingine, Mwalimu Samson Sombi amesema uteuzi wa Rais Samia unaonesha kwamba, mbali na majukumu ya kisiasa wanayopewa viongozi, pia suala la uzalendo wao unangaliwa na namna wanavyotunza siri za Serikali.

Mwalimu Sombi amesema kazi kubwa ya Baraza la Mawaziri ni kumshauri Rais, hivyo wakati wa uteuzi ni lazima aangalie nani aliyekuwa akimsaidia kwenye ushauri, akisisitiza wengi waliorejea kwenye nafasi zao Rais aliwaangalia zaidi mchango wao.

Manaibu waziri waliopanda

Mbali na sura mpya kuteuliwa uwaziri pamoja na mawaziri wa zamani kurejea, Rais Samia amewapandisha manaibu waziri kuwa mawaziri kamili. Miongoni mwao ni Deus Sangu ambaye amekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano.

Mwingine ni Judith Kapinga, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati, sasa anakuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na naibu wake ni Patrobas Katambi.

Akizungumzia kupandishwa kwa manaibu hao, Sabatho Nyamsenda kutoka UDSM, amesema suala la kupanda ngazi ya kiuongozi linapaswa kuendana na rekodi za mhusika juu ya utendaji wake wa nafasi aliyotoka.

“Kupandishwa cheo kunatokana na uwezo na rekodi ya mtu na utendaji wake na vigezo vinavyoonekana vinavyoweza kupimwa. Mfano, nchi ya China, mtu akitaka kwenda ngazi ya juu, kazi yake inaonekana kwa kupimwa alichofanya,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Wakili Onesmo Kyauke, amesema inaonekana wakuu hao wa mikoa walifanya vizuri katika mikoa waliyokuwa wakiongoza, ndiyo maana wamepata nafasi hiyo.

“Anayeteua anaangalia utendaji wao huko nyuma, na ukiangalia kazi ya uwaziri zaidi ni kwenye sera, ingawa majukumu yanasimamiwa na Katibu Mkuu,” amesema.

Katika baraza lenye mawaziri 27, Rais Samia amewateua mawaziri wanawake wanne kutoka watano waliokuwapo kwenye baraza lililopita.

Walioteuliwa sasa ni Dk Ashatu Kijaji (Maliasili na Utalii), Judith Kapinga (Viwanda na Biashara), Dk Dorothy Gwajima (Maendeleo ya Jamii), na Angellah Kairuki (Mawasiliano na Teknolojia ya Habari).

Akizungumzia suala la jinsia, Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Dk Ananilea Nkya, amesema kuteuliwa kwa wanawake wachache kuwa mawaziri haimaanishi hakuna wanawake wenye uwezo wa kuongoza.

Amesema hilo linaweza kuwa limesababishwa na wanawake wenye uwezo wa kuwa viongozi kutojihusisha kikamilifu na masuala ya siasa.

Amesisitiza kwamba uwepo wa Katiba bora unaweza kuamsha ari ya wanawake wenye uwezo wa kuongoza kuingia katika masuala ya siasa.

“Tatizo hapa ni Katiba. Tukipata katiba bora, wanawake wenye uwezo wa kuongoza watajitokeza kwa wingi na kugombea,” amesema.

Naye, kada wa CCM, Angela Akilimali amepongeza hatua ya wanawake kuendelea kuaminiwa na kupewa wizara nyeti zinazogusa wananchi moja kwa moja.

Amesema amevutiwa kuona sura mpya za baadhi ya wanawake ambao pia ni vijana wameteuliwa katika baraza hilo.

Ametoa wito kwa wanawake hao walioteuliwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kusaidia ukuaji wa maendeleo nchini.

“Kwa kuwa wameteuliwa katika wizara zinazogusa moja kwa moja jamii, wanatakiwa kufanya kazi nzuri kuondoa changamoto za jamii,” amesema.