Pacome, Doumbia wamtikisa Kocha Mreno

KIKOSI cha Yanga kimeshavuka bahari ya Hindi na kutua visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mwisho ya kukabiliana na Far Rabat ya Morocco katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha wa timu pinzani ameanza kuingiwa ubaridi mapema.

Yanga iliyopo Kundi B sambamba na JS Kabylie ya Algeria na Al Ahly ya Misri itakuwa wenyeji wa Far Rabat Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kabla ya kuifuata JSK Algeria na mapema mwakani kucheza nje-ndani dhidi ya wababe wa Afrika kutoka Misri.

Wakati kocha Pedro Goncalves akiendelea kujipanga kwa ajili ya pambano hilo litakalopigwa kuanzia saa 10:00 jioni, kocha wa Far Rabat, Alexandre Santos, raia wa Ureno kama ilivyo kwa Pedro, amekiri anaumizwa kichwa na namna ya kuwakabili wenyeji, huku akitaja eneo tishio kwao ni kiungo kinachoongozwa na kina Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Mohamed Doumbia.

Santos aliyekuja mara ya mwisho nchini msimu uliopita ikiwa na CS Sfaxien ya Tunisia na kupoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Simba Desemba 15, 2024, ameliambia Mwanaspoti Yanga ni moja ya timu tishio, ikiwa na nyota wenye unyumbulifu na wasumbufu bila kuwataja majina.

PACO 03


Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo ya Jumamosi, Santos alisema maandalizi dhidi ya Yanga yameshindwa kuwa mazuri sana kutokana ugumu wa kupata ubora sahihi wa wapinzani wao hao ambao watakuwa wenyeji wao.

Santos alisema kitu pekee ambacho amekiona kwa Yanga kwa kuangalia mechi zao zilizopita aligundua timu hiyo ina viungo bora na lazima wajipange sawasawa kuwadhibiti watakapokutana kwenye Uwanja wa Amaan katika mechi ya kwanza ya Kundi B.

Kocha huyo, alisema ugumu zaidi unatokana na Yanga sasa kuwa chini ya kocha mpya ambaye anamfahamu akiwa ni raia mwenzake kutoka Ureno, Pedro Goncalves, lakini bado hajapata kuona ubora sahihi wa kikosi hicho hadi sasa.

“Naweza kusema kitu usiamini, lakini imekuwa vigumu sana kuwasoma wenzetu, kweli namjua kocha Pedro (Goncalves) ni kocha mzuri sana ila bado hatujaona ubora wa kikosi chake ambao ungetusaidia kujua uhakika wa namna wanavyocheza,” alisema Santos na kuongeza;

PACO 04


“Timu yao (Yanga) ni nzuri ukiangalia mechi zilizopita utaona wana wachezaji wenye ubora ambao lazima tuwe nao makini, eneo bora sana kwao ni katikati, kuna wachezaji wabunifu sana wanaweza kusababisha lolote wakati wowote ukifanya makosa.”

Eneo hilo la kiungo kwa Yanga lina mastaa kama Duke Abuya, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Lassine Kouma, Mohamed Doumbia, Pacome Zouzoua na wengine ambao wameiwezesha timu hiyo kuzitesa timu pinzani katika mechi za kimataifa na hata za Ligi Kuu ikiongoza msimamo.

PACO 01


Santos alisema hatua nyingine inayomsumbua ni ubora wa Yanga ikiwa nyumbani akisema hilo limekuwa gumu, sio Yanga pekee kwani aliwahi kukutana na wakati mgumu alipokutana na Simba akipoteza dakika za mwisho.

“Mechi kumi zilizopita wameshinda tisa na kupoteza moja, hii ni rekodi bora ambayo lazima ujue ugumu wa mpinzani unayekutana naye akiwa nyumbani ana ubora gani, timu nyingi za Tanzania sio rahisi kupoteza nyumbani,” alisema Mreno huyo na kuongeza;

“Bado nakumbuka rafiki yangu, ile mechi dhidi ya Simba nilipokuja hapo, niliona kabisa inaisha kwa sare, lakini tukafanya makosa huku mwamuzi naye alituumiza sana akasababisha tukaruhusu bao la pili, sio rahisi sana kupata matokeo ukiwa hapo Tanzania, ila naiamini timu yangu tutajaribu kufanya kitu tofauti, tunataka kuanza vizuri.”

Yanga iliyofuzu makundi ikiwa ni mara ya tatu mfululizo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na ya nne mfululizo ukijumuisha na Kombe la Shirikisho Afrika ambako ilifika fainali 2022-23, msimu huu ilizing’oa Wiliete Benguela ya Angola katika raundi ya kwanza ya mchujo kwa mabao 5-0 kabla ya kuifyatua Silver Strikers ya Malawi kwa mabao 2-1 mechi za raundi ya pili ya mtoano.