Polisi nchini yamkamata Sajenti wa Jeshi la Marekani akiwa na mabomu manne

Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Tarime–Rorya mkoani Mara limemkamata Sajenti wa Jeshi la Marekani, Charles Onkuri Ongeta (30), mwenye uraia pacha wa Marekani na Kenya, baada ya kukutwa na mabomu manne ya kurushwa kwa mkono aina ya CS M68 katika eneo la mpakani Sirari.

Tukio hilo limetokea jana Jumapili, Novemba 16, 2025, saa 6:00 mchana, wakati askari wa ulinzi mpakani walipomuhoji mtuhumiwa aliyekuwa akiingia Tanzania akitokea Kenya na gari aina ya Toyota Land Cruiser.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime–Rorya, Mark Njera, imeeleza kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa kumetokana na umakini wa askari waliokuwa doria mpakani.

“Askari wetu walifanya ukaguzi wa kawaida na ndipo walipobaini uwepo wa mabomu manne ya kurushwa kwa mkono ndani ya gari alilokuwa akiendesha mtuhumiwa,” amesema Kamanda Njera.

Ameongeza kuwa silaha hizo ni marufuku kuingizwa nchini kwa mujibu wa sheria za Tanzania hata kama angekuwa ameomba kibali maalumu.

“Kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa silaha, mabomu ya aina hii hayaruhusiwi kabisa kuingizwa nchini. Hata kama angeomba kibali, asingeruhusiwa kuyapitisha,” amefafanua.

Kamanda Njera amesema uchunguzi wa awali unaendelea, ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi na kumuhoji mtuhumiwa, ili hatua za kisheria zichukuliwe  baada ya taratibu kukamilika.

 “Tunachukua hatua zote za kipolisi. Mara tu uchunguzi utakapokamilika, tutawasilisha jalada kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi,” amesema.