Rasilimali watu sekta ya afya itakavyoboresha maisha

Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya afya Tanzania, wamesema kwenye utoaji na wigo wa huduma za afya bado kuna pengo kubwa, wakisisitiza namna ongezeko la ajira za wahudumu wa afya litakavyosaidia kuboresha maisha ya Watanzania.

Wamesema licha ya Serikali kuboresha na kuongeza miundombinu katika sekta hiyo bado vifaa vingi vinashindwa kutumika, huku ugunduzi wa mapema kwa magonjwa hasa yasiyoambukiza upo kwa kiwango cha chini kwa kukosa wataalamu hasa maeneo ya pembezoni.

Akilihutubia Bunge la 13 na kulizindua, Novemba 14, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alisema ataanza na masuala aliyowaahidi wananchi ndani ya siku 100 za mwanzo za kazi kuwa Serikali atakayoiunda itawajibika na kuendelea na mageuzi ya sera zinazogusa masilahi na ustawi wa maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Tuliahidi kutoa ajira kwa fani za sekta ya afya. Leo ikiwa ni siku ya 12 tangu muhula huu wa pili wa awamu ya sita uanze, tayari tumeshatangaza nafasi za ajira 5,000 za watumishi wa afya. Hatua hii ni ya mwanzo kujibu kiu ya wananchi ya kuboresha huduma za afya,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo wadau wa sekta hiyo wamesisitiza kuwa ili hayo yafanikiwe, Serikali haina budi kuangalia namna itakavyoongeza watumishi katika sekta ya afya ili kufanikisha malengo ya kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema sekta ya afya nchini ni kubwa inayochagiza maendeleo, na kwa kuwa afya ni mtaji, Rais Samia anapaswa kuongeza mengi zaidi ya aliyoyasema kwenye sekta hiyo.

Amesema bado kuna kazi ya kufanya kwenye utoaji na wigo wa huduma bado kunahitajika vifaa vya kisasa ili wataalamu waweze kufika kwenye vituo vyote vya kutolea huduma katika hospitali zote za rufaa waweze kutoa tiba za moyo, tiba ya mishipa zote kuna hitaji ya kusomesha wataalamu zaidi.

“Vituo vyote vya kutolea huduma vilivyopo ngazi ya msingi bado havina wataalamu, ajira zilizotolewa ni chache tuzingatie watumishi wa kutosha. Watumishi wa afya 5,000 aliosema atapeleka haimalizi hitaji ni tone kwenye bahari.

“Watu wanatakiwa wafike vituoni wakute kila kitu upatikanaji wa wahudumu, tiba ikiwemo ugunduzi wa magonjwa katika hatua za awali na dawa, tumeshuhudia baadhi ya maeneo vifaa vipo lakini vinabaki katika maboksi sababu hakuna wataalamu wa kuvitumia,” amesisitiza na kuongeza.

“Tupate ufafanuzi wa kutosha kuhusu ajira maana zilizotangazwa ni marejesho ya waliofariki, waliostaafu ajira mpya hasa ni kiasi gani. Licha ya wataalamu waliosomeshwa kubaki mtaani, wananchi pembezoni wanahitaji huduma.”

Mwenyekiti wa watoa huduma za afya binafsi (Aphtha), Dk Egina Makwabe amesema wataalamu wa afya ni tatizo, ambalo wamekuwa wakilisemea kwa miaka mingi na waliopo ni wa kupokezana kati ya hospitali za umma na binafsi.

Amesema tatizo hilo limekuwa likiwaumiza zaidi watoa huduma binafsi ambao huwachukua wahitimu na kuwapa mafunzo kwa vitendo kisha huwaajiri, kabla ya kupata ajira serikalini.

“Tunapata hasara kubwa sana, maana wakiwachukua sisi tunaanza upya kufundisha wengine. Wahitimu ni wengi na kwa sasa kila mwaka madaktari 1,500 wanahitimu, lakini wengi wapo vijiweni na huku pembezoni watu wanawahitaji wataalamu,” amesema.

Dk Makwabe amesema nchi Ina upungufu mkubwa wa watumishi wa afya kwa kada zote, suala ambalo ameshauri Serikali iangalie namna itakavyoweza kulishughulikia ili kuboresha afya za Watanzania.

Awali, Dk Nkoronko amesema katika hotuba yake, kuna mambo mengi ambayo Rais ameyaainisha ambayo wataalamu wanahitaji ufafanuzi zaidi.

“Kuna mambo mengine tumeona mwanga mdogo kwa mbali tunasubiri ufafanuzi zaidi ili tuone mwelekeo wa sekta ya afya nchini kama kuimarisha hospitali ya Muhimbili kivipi? Tunataka tujue uimarishaji ni upi?

“Uwezo wetu wa kuhimili magonjwa ya mlipuko ukoje, amesema atajenga hospitali ni jambo moja je magonjwa yakilipuka Mbeya tutawapekea huko?”

Dk Nkoronko amesema bado Watanzania wanahitaji kuona uwepo wa miundombinu ya kupunguza ajali barabara ziwe na maeneo ya waendesha baiskeli, mitaro iliyofunikwa.

“Tunataka tuone huduma bora za tiba na kinga kwa vyakula vinavyoingizwa nchini sababu lishe inaathiri kwa kiasi kikubwa, Rais amesema anatamani mifumo isomane lini itasomana, ifanye kazi kwenye vituo vyote nchini,” amesema.

Akilihutubia Bunge Novemba 14, 2025 Rais Samia aligusia kunajiandaa kuanza kwa majaribio ya Bima ya Afya kwa Wote. Serikali kuchukua mapendekezo ya namna ya kufanikisha majaribio hayo, kwa Bunge mapendekezo yatakayokuwa mwanzo wa mageuzi katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote nchini.

Dhamira ya kuviunganisha vituo vya huduma za afya kidijitali na kuhakikisha vinakuwa na vifaa na huduma za viwango stahiki kwa kila ngazi husika.

Kuweka viwango vinavyofanana ili watumiaji wa bima ya afya mijini na vijijini wawe na huduma zinazolingana.

Wizara ya Afya kusimamia maelekezo ya kutozuiwa maiti kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, wakati familia zikiendelea na taratibu za kulipa deni la matibabu kwa njia zinazolinda utu wao.

Wananchi kuweka kipaumbele kwa afya zao, kwa kila mmoja kuwa na bima ya afya pamoja na wanaomtegemea.

Kukamilisha ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati zinazojengwa kote nchini.

Kuendelea kuboresha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuongeza uwezo wake kutoka vitanda 1,435 vya sasa hadi vitanda 1,757 ifikapo 2030. Itakapokamilika, itaweza kutoa huduma za kibingwa na kuwa hospitali ya kutumainiwa na kukimbiliwa katika Afrika ya Mashariki.

Kuongeza huduma za kibingwa za afya kwenye hospitali za rufaa za Mikoa na hospitali za rufaa za Kanda, ili tuwapunguzie gharama wananchi kutafuta huduma za rufaa nje ya mikoa yao. Badala ya watu kuzifuata huduma, huduma ziwafuate.

Kuendelea kuwekeza katika kujenga uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Kujenga hospitali kubwa ya Kitaifa ya magonjwa ya mlipuko mkoani Kagera.

Kuongeza uwezo wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kupunguza uagizaji na kupunguza gharama za matibabu. Kuvihakikishia viwanda vya ndani soko la uhakika kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

Kukuza utafiti, utambuzi na utoaji wa ithibati wa dawa zetu za asili.

Kujielekeza zaidi kwenye kinga (preventive medicine) tofauti na sasa ambapo tumejikita zaidi kwenye tiba (curative medicine) pekee.

Pia Rais Samia alisema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya na ahadi yake ni kuendeleza ushirikiano huo.