Tato yataka Serikali kuimarisha meza ya majadiliano ili kulinda utalii endelevu

Arusha. Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (Tato) kimeiomba Serikali kuimarisha meza ya majadiliano na wananchi pamoja na wadau muhimu ili kulinda uthabiti wa sekta ya utalii.

Ombi hilo limetolewa kufuatia tishio la uvunjifu wa amani zilizotokana na vurugu katika baadhi ya maeneo nchini kati ya Oktoba 29 na 31 mwaka huu.

Chambulo amesema hayo wakati Tanzania tayari imevuka lengo lake la utalii kwa mwaka 2025, ikifikisha watalii milioni 5.3 na mapato ya dola bilioni 4 hadi kufikia Aprili 2025, zaidi ya makadirio ya awali ya watalii milioni tano.

Serikali sasa imeongeza malengo yake na inalenga kuvutia watalii milioni 8 kwa mwaka ifikapo 2030, lengo linalosukumwa na mageuzi ya sekta ya utalii, maboresho ya miundombinu na jitihada kubwa za uhamasishaji.

Akizungumza jijini Arusha, leo Novemba 17,2025, Mwenyekiti wa Tato, Willy Chambulo, amesema sekta ya utalii imeendelea kuwa imara licha ya mvutano wa kisiasa uliosababisha sintofahamu katika baadhi ya maeneo ya mijini.

Mwenyekiti wa TATO, Willy Chambulo

“Utalii ni sekta nyeti sana, na tunashukuru kwamba iliendelea kuwa thabiti hata wakati wa sintofahamu,” amesema Chambulo na kuongeza; “ Lakini hatupaswi kulichukulia poa jambo hili bali Serikali inapaswa kuwasikiliza wananchi kwa makini na kushughulikia hoja zao kupitia majadiliano yenye utaratibu ili matukio kama haya yasitokee tena.”

Vurugu hizo zilizotokea wiki ya uchaguzi zilisababisha vifo na uharibifu wa miundombinu ikiwemo vituo vya mafuta, vituo vya polisi, hoteli na nyumba za wageni katika baadhi ya maeneo.

Amesema kuwa ingawa ni baadhi ya maeneo, lakini  itoshe  kuonyesha umuhimu wa kuboresha njia za mawasiliano kati ya mamlaka na wananchi.

Chambulo pia alionya dhidi ya matumizi makubwa ya nguvu katika kudhibiti maandamano, akisisitiza kuwa ushirikiano wa amani ni mbadala bora zaidi wa kudumisha utulivu wa Taifa.

“Maandamano hutokea katika kila nchi, lakini waandaaji wanapewa ulinzi, njia zinaratibiwa na taratibu kufuatwa, ili maandamano yabaki kuwa ya amani,” amesema na kuongeza.

“ lakini kitendo cha kuzuiwa kwa nguvu bila majadiliano kunachochea migongano na waandamanaji kutumia nguvu kufanikisha jambo lao na hapo ndio kutoelewana inapotokea.”

Aidha, aliwahimiza wananchi na wadau wa sekta zote kulinda amani ya Taifa, akionya kuwa vurugu hazichagui, zinawaathiri wote na hatimaye kuathiri uchumi mzima, ikiwa ni pamoja na utalii.

Aidha taarifa rasmi ya tathimini kutoka Tato imeeleza matukio hayo hayakuathiri maeneo ya utalii.

Amesema hifadhi na maeneo makuu ya utalii kama Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Tarangire, Ruaha, Hifadhi ya Taifa Nyerere, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar yalisalia salama, tulivu na yakiwa yanatekeleza shughuli zote kama kawaida.

“Safari, ndege za ndani, malazi na usafiri wa watalii vilikuwa vinaendelea bila usumbufu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

 “Ujio wa watalii unaendelea kwa kasi, huku watoa huduma, hoteli na hifadhi za taifa wakipokea wageni kama kawaida, Tanzania bado ni moja ya maeneo salama na yenye utulivu zaidi barani Afrika kwa ajili ya utalii wa safari, ikisaidiwa na mawasiliano ya karibu kati ya chama, mamlaka za utalii, hifadhi za taifa, vyombo vya usalama, Serikali za mitaa na watoa huduma,” imeeleza.

Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Solo Adventure, Athumani Njiku, amesema kuwa Tanzania bado inaweza kufanikisha malengo yake ya utalii kwa kudumisha amani iliyopo na kuhakikisha haki kwa wananchi wake.

“Amani bado ipo, na uzuri wa nchi unaendelea kuvutia wageni, kikubwa ni kutoruhusu vurugu zichukue nafasi, na vyombo vya habari vya kimataifa vinaporipoti vurugu hivyo havipaswi kunyamaziwa bali wapewe taarifa halisi ili kuzuia upotoshaji.”