Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kufanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri kuanzia sasa, wachambuzi wameiangazia nafasi ya waziri wa fedha huku wakiainisha mambo anayotakiwa kuyasimamia ili kukuza uchumi wa Tanzania.
Rais Samia ameshamteua Dk Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu na kuthibitishwa na Bunge kisha kuapishwa Novemba 14, 2025 kushika wadhifa huo.
Wakati mkuu huyo wa nchi tayari akiwa ameshalihutubia na kulizindua Bunge la 13, kinachofuata ni uundwaji wa Baraza la Mawaziri.
Miongoni mwa wizara nyeti ni ya fedha iliyokuwa ikiongozwa na Dk Mwigulu na kwa baraza lijalo, litakuwa na waziri mpya.
Wengi wanatajwa lakini Rais Samia anamjua mtu sahihi wa nafasi hiyo.
Mwananchi imezungumza na wadau wabobezi wa uchumi na kuainisha masuala kadhaa ambayo waziri mpya wa fedha anapaswa kuyatilia mkazo.
Miongoni mwa mambo hayo ni kusimamia ukusanyaji wa mapato, kupunguza viwango vya tozo, kujenga uchumi jumuishi, kusimamia Dira ya Taifa 2050 na kupunguza matumizi ya Serikali pamoja na kudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma.
Akizungumza na Mwananchi, leo Novemba 17, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari amesema waziri wa fedha ajaye anapaswa kuhakikisha mfumo wa makusanyo ya kodi unafanyiwa marekebisho kutokana na mapendekezo ya Tume iliyoundwa na Rais.
“Hiyo itasaidia kupanua wigo wa kodi, wananchi watalipa kodi kwa hiyari na viwango vya kodi na tozo vipunguzwe ili iwe rahisi, hii itasaidia kuongeza wigo na makusanyo yatakuwa ya kutosha,” amesema Dk Mmari.
Jambo jingine, amesema anapaswa asimamie nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali ili zifanye kazi iliyokusudiwa, matumizi yasiyo ya lazima yapunguzwe na ubadhirifu wa fedha za umma udhibitiwe.
Pia, Dk Mmari amemtaka atakayeteuliwa, aangalia deni la Taifa ili lisikue bila sababu za msingi, lisipite viwango vya uhimilivu.
Amesema hilo litafanya makusanyo yasitumike kulipa madeni, bali kutoa huduma kwa wananchi.
“Ahakikishe mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa rafiki, yasiyo na usumbufu wala mazingira ya rushwa ili tuweze kuvutia uwekezaji na sekta binafsi ikue na kutoa ajira kwa vijana wengi,” amesema Dk Mmari.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi amesema waziri wa fedha ajaye anakabiliwa na kibarua cha kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050.
Amesema anatakiwa kuhamasisha ukuaji wa uchumi utakaolifikisha Taifa kule linakotaka kufika ifikapo mwaka 2050.
Amemtaka ashirikiane kwa karibu na mtangulizi wake, Dk Mwigulu ili aendeleze pale alipoishia kufikia malengo ya kitaifa.
“Rais atafute mtu ambaye ni mwanauchumi ili iwe rahisi kwake kuhakikisha mambo yanayotarajiwa kufanyika kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050 yanafikiwa. Atufikishe kwenye uchumi wa kati wa juu,” amesema mwanazuoni huyo.
Profesa Moshi amesema waziri wa fedha ahakikishe anajenga uchumi jumuishi na hilo halijafanikiwa kwa sababu asilimia 64 ya kaya za Watanzania zinategemea kilimo na kwa kuwa watu wengi wanategemea kilimo, maana yake siyo chenye tija.
“Jambo la kufanya ni kuhakikisha kilimo kinakuwa chenye tija na kitakuwa na tija kama tutahamasisha kilimo cha umwagiliaji. Tanzania tuna vyanzo vingi vya maji, kwa hiyo tuanze kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji,” amesema.
Vilevile, ameshauri waziri huyo asimamie kupunguza utegemezi wa dola kwa sababu inaathiri uchumi kwa kupanda kila wakati.
Profesa Moshi amesema mshirika mkubwa wa Tanzania ni China, hivyo wajaribu kutumia sarafu zao, yaani Shilingi ya Tanzania na Yuan ya China.
“Tufanye kama yanavyofanya mataifa ya Brics, wao wameachana na dola, wanatumia sarafu zao kufanya biashara. Tutumie nafasi yetu ya kuwa na Wachina tuhakikishe tunafanya mambo yetu kwa sarafu zetu wenyewe,” amesema.
Mchambuzi wa uchumi, Profesa Haji Semboja amesema anayeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, kutokana na wadhifa wake, inabidi ahakikishe fedha zenyewe zinatafutwa katika vyanzo vyote vya fedha.
“Source (chanzo) nzuri kwa Serikali ni kuhakikisha fedha zinatafutwa katika hizi natural resources (mali asili) tulizokuwa nazo na vyanzo vya watu wenyewe.
“Hizo natural resources zitatuletea pesa nyingi, kama tukizimiliki, kusimamia na kuziendesha wenyewe, lakini tukianza ‘upuuzi’ wa kusema tunawakaribisha watu wa nje halafu wanachukua hizo resources kama diamond, gold (dhahabu), mafuta aua chochote.
“Halafu tunategemea kodi, huko kutafanya tuwe maskini kwa sababu hakutakuwa na uhusiano kati ya rasilimali tulizokuwa nazo na hali ya pesa tuliyokuwa nayo,” amesema.
Amesema waziri huyo anapaswa kuangalia hilo, akibainisha kwamba shida ni tafsiri ya kuzitafuta hizo fedha, akisisitiza lazima Tanzania yenyewe ndiyo iwe mmiliki, isimamie na kuendesha rasilimali ilizonazo.
“Lazima wenyewe tuzimiliki, tuzisimamie na tuziendeshe, naamini tukifanya hivyo hatutakuwa na tatizo, kwa kufanya wewe mwenyewe utakuwa na credibility (ubora) nje, kwa hiyo mikopo ya kibiashara tunaweza kuichukua tu,” amesema.
Profesa Semboja amegusia pia mpango wa Serikali, akibainisha nao unapaswa kutafsiri sera akisisitiza nchi haiwezi kuwa na mpango ambao hautekelezi sera.
“Baada ya kuwa na mpango, pawepo na uhakika kwamba system zote za monitoring control, evaluation (tathimini) na Oditing (ukaguzi) zinasahihisha na kuweka vizuri vitu vyote vinavyotakiwa vipatane na resorces (rasilimali) tulizokuwa nazo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Pia, kwa zile taasisi ambazo zipo chini ya Wizara ya Fedha, mfano Benki Kuu (BoT) na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania ziwe na watu sahihi kulingana na professional zilizopo kwenye taasisi hizo,”amesema Profesa Semboja.
Amesema kufanikisha hilo, ni lazima rasilimali nguvu kazi kwenye taasisi hizi ziweze kusaidia mfumo mzima na zisiwe ni nafasi za ‘kupeana’ kwa kufahamiana nani ni nani au watu kupelekwa kufanya kazi licha ya kwamba, si mahitaji ya taasisi.
Mchumi mwingine, Oscar Mkude amesema vipaumbele vipo vingi kwenye Taifa, akibainisha Watanzania wengi wanatamani kuona nchi yao ikiwaletea matumaini.
Amesema Wizara ya Fedha ndiyo msimamizi wa rasilimali, matumizi ya makusanyo na fedha za umma.
“Matumizi ya fedha za umma ni swali linaloleta changamoto, maswali yamekuwa yakijitokeza wengi wakiona matumizi hayaleti tija, masuala ya kupena zabuni na vitu kama hivyo.
“Pamoja na hayo, wizara ya fedha kama wasimamizi wa fedha za umma na rasilimali za nchi, tunategemea kuweka mkazo katika matumizi ya fedha za umma, mfano kuna maeneo kama magari, Watanzania wengi ni maskini, lakini haipendezi kuona viongozi wanaendesha magari ya kitajiri.
“Kuna nchi ni matajiri, lakini viongozi wao wanaendesha magari ya kawaida, matumizi ya umma ikiwamo ya magari ni makubwa, tunatamani kuona hivyo vinapungua fedha za umma zitumike kwenye maendeleo ya umma.
Amesema kuna haja ya kudhibiti matumizi ya fedha za uma na kuweka kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya maendeleo, akibainisha waziri wa fedha ajaye akifanikisha hilo hata imani ya wananchi itakuwepo kwa viongozi wao.
Walichokisema wafanyabiashara
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Khamis Livembe amesema wanatarajia waziri wa fedha ajaye atavaa viatu vya mtangulizi wake ikiwamo kujadiliana na wafanyabiashara.
“Mwigulu tulikuwa na vikao naye vingi na mara zote kukiwa na jambo, tunakaa naye na kulimaza mezani, naye akiwa na jambo jipya tunalimaliza mezani.
“Kipindi cha miaka minne mfululizo (Mwigulu) akiwa waziri wa fedha, yalifanyika makongamano ya kodi, akipokea maoni ya wadau wote wa kodi, kabla ya kwenda kwenye bajeti,” amesema mwenyekiti huyo.
“Hiyo ilitusaidia kuondoa sintofahamu sababu hata zile kodi ambazo zipo watu huwa hawaridhiki nazo, lakini mnapokutana akawaeleza, hili tumefanya hivi kwa sababu ya moja mbili tatu, watu wanaelewa na kuridhika.”
Amesema Mwigulu alipokuwa waziri wa fedha makusanyo yaliongezeka, hivyo kama jumuiya ya wafanyabiashara, wanategemea atakayeteuliwa kwenye nafasi hiyo, pia, ataongeza makusanyo na kuendeleza yale mazuri yote yaliyofanywa na mtangulizi wake.
“Tunategemea afanye hivyo, tuna matarajio anayekuja atavaa viatu vya mtangulizi wake ambaye naye yupo, hivyo atamuongoza, kama jumuiya ya wafanyabiashara hatutarajii kupata waziri wa fedha ambaye tutasumbuana naye,” amesema Livembe.
