Dar es Salaam. Saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza baraza jipya la mawaziri, baadhi ya mawaziri waliokuwemo kwenye baraza lililopita ambao sasa ni wabunge wa kawaida, wamefunguka wakitoa pongezi na shukurani.
Miongoni mwa mawaziri walioachwa na wizara zao kwenye baraza lililopita ni: Dk Doto Biteko (aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati), Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani), Jenista Mhagama (Afya), Dk Seleman Jafo (Viwanda na Biashara), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii) na Dk Damas Ndumbaro (Katiba na Sheria).
Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, baadhi ya mawaziri waliokuwa wameshiriki baraza lililopita wameandika wakishukuru na kuahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa sasa.
Kupitia Instagram yake, Hussein Bashe, aliyekuwa Waziri wa Kilimo kabla ya wizara hiyo kupewa Daniel Chongolo, ameandika kuwa anashukuru kwa kuaminiwa katika kipindi chote alichotumikia katika nafasi hiyo.
“Salaam ndugu zangu. Natumia nafasi hii kumshukuru Allah kwa kila jambo na kwa baraka zake katika safari yangu ya utumishi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu_Hassan kwa imani kubwa aliyonionyesha katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi kama naibu waziri, na baadaye kuniteua kama waziri wa kilimo.
“Ni heshima niliyothamini kwa moyo wangu wote, na ninaendelea kuwa mwenye shukurani kwa nafasi hiyo ya kuwatumikia Watanzania. Natoa pongezi za dhati kwa ndugu Daniel_Godfrey_Chongolo kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo. Namfahamu kama mkulima na mzalendo. Nina uhakika atamsaidia mheshimiwa Rais kutimiza matarajio ya Watanzania. Vilevile, nampongeza ndugu yangu David Silinde kwa kuendelea kuaminiwa kama Naibu Waziri. Sina mashaka naye mzazi najua atakuwa msaada mkubwa kwa waziri wake.
“Nawashukuru pia watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano wa hali ya juu mlionipa katika kipindi cha miaka sita. Nawatakia heri na fanaka katika kuendelea kutekeleza majukumu yenu ya kuwatumikia Watanzania. Asanteni sana.”
Kwa upande wake Innocent Bashungwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Wizara aliyopewa Boniface Simbachawene ameshukuru akisema “Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kipindi tulichopata kuwatumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali.
“Naomba kumshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan kwa fursa adimu uliyonipa katika vipindi mbalimbali kuwatumikia Watanzania. Naomba nikuahidi tutaendelea kuunga mkono juhudi na maono mazuri ya uongozi wako pamoja na Serikali ya awamu ya sita unayoiongoza.
“Naomba pia kuwashukuru wananchi na matajiri wangu wananchi wa Jimbo la Karagwe kwa ushirikiano na imani kwangu. Sasa nimepata muda wa ziada wa kukaa jimboni ili kazi iendelee na kwa kasi zaidi. Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”
Dk Damas Ndumbaro aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, wizara aliyopewa Juma Homera amesema; “Napenda kutoa shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini katika kipindi chote kuhudumia wananchi wenzangu katika nafasi ya waziri katika sekta mbalimbali, fursa hii ilikuwa heshima kubwa kwangu, na imenipa nafasi ya kuwahudumia wananchi wetu kwa moyo, uadilifu na kujitolea.
“Nawashukuru sana wananchi wote, viongozi wenzangu, watumishi wa umma, na wadau mbalimbali ambao tumefanya kazi kwa ukaribu.
“Tumeshirikiana kwa bidii kutekeleza majukumu ya kuwatumikia Watanzania na kuleta maendeleo katika sekta tulizokuwa tukisimamia.
“Ninaendelea kuwa mtumishi wa wananchi, mzalendo na mshiriki katika jitihada za kuijenga Tanzania tunayoitamani. Ninawapongeza na kuwatakia kila la heri wote walioaminiwa na kuteuliwa katika kuwahudumia Watanzania.
Kazi na Utu Tunasonga Mbele,” ameandika katika ukurasa wake wa Instagram.