‎Washitakiwa 11 wa maandamano wafikishwa kortini, kesi yapigwa kalenda

‎Mwanza. Watuhumiwa 11 kati ya 172 wanaokabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya uharibifu wa mali ya umma, unyang’anyi wa kutumia silaha na kufanya maandamano bila kibali katika vurugu zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, kesi yao imepigwa tena kalenda hadi Novemba 26, mwaka huu.

‎Watuhumiwa hao ni miongoni mwa 172 waliofunguliwa mashtaka hayo katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza kutokana na matukio yaliyotokea kati ya Oktoba 29 hadi 31, mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.

‎Watuhumiwa wengine wenye kesi za namna hiyo zilizotokana na matukio yaliyotokea kati ya Oktoba 29 hadi 31, mwaka huu, kesi zao zitatajwa kwa mara ya pili Novemba 19, 20 na 21 mwaka huu mahakamani hapo.

‎Ambapo, walisomewa hati ya mashtaka yanayowakabili kwa mara ya kwanza Ijumaa Novemba 7, 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Mwanza.

‎Watuhumiwa hao 11 wanakabiliwa na mashtaka mawili ya uharibifu wa mali kwa kuchoma moto vitu kinyume na kifungu cha 319 (a) (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Baadhi ya watuhumiwa wanaokabiliwa na mashtaka ya uharibifu wa mali na unyang’anyi wa kutumia silaha katika matukio yaliyotokana na uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025. Picha na Maktaba

‎Pia, wanakabiliwa na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

‎Shauri hilo limetajwa leo Novemba 17, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Ramla Shihagilo, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mahembega Elias ameiomba Mahakama kuahirisha shauri hilo kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

‎Baada ya hoja hiyo, Hakimu Shihagilo amehirisha shauri hilo hadi Novemba 26, 2025 litakapotajwa tena, kwa kuwa upelelezi haujakamilika huku watuhumiwa wakiendelea kubaki mahabusu hadi tarehe hiyo kutokana na mashtaka yao kutokuwa na dhamana.