JKT Queens inajiandaa kurejea nchini baada ya kung’olewa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa timu za wanawake (WCL), lakini kuna Watanzania wawili wanaokipiga klabu ya FC Masar ya Misri watakaokuwa uwanjani usiku wa leo katika mechi za nusu fainali.
Wawakilishi hao wa Tanzania walipangwa Kundi B na kumaliza nafasi ya tatu ikitoka sare mbili na kupoteza mechi ya mwisho dhidi ya watetezi, TP Mazembe ya DR Congo iliyofuzu hatua hiyo ambayo itakuwa uwanjani kuvaana na FAR Rabat ya Morocco.
Hata hivyo, wenyeji Masar watashuka uwanjani kuanzia saa 1:00 usiku kuvaana na Asec Mimosas ya Ivory, huku wachezaji wa Kitanzania, Hasnath Ubamba na Violeth Nickolaus walioipeleka timu hiyo nusu fainali wanatarajiwa kuendelea kuipigania timu hiyo ili kusaka tiketi ya fainali.
Hii ni mara ya kwanza Masar na Asec kukutana, huku chama la Watanzania hao ikiwa mara ya pili mfululizo linashiriki mashindano hayo, kwani mwaka jana lilimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kutolewa katika nusu fainali na AS FAR.
Kiujumla hii ni nusu fainali ya pili kwa Masar na kama itavuka kwenda fainali basi itakuwa mara ya kwanza kucheza hatua hiyo, lakini kwa Asec hii ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo tangu ilipoasisiwa mwaka 2021.
Licha ya ugeni katika mashindano hayo, Asec imetinga nusu fainali baada ya kumaliza kinara wa Kundi B ikimaliza na pointi saba, mechi ya kwanza iliwatandika watetezi TP Mazembe kwa bao 1-0, kisha ikatoa sare ya 1-1 na JKT Queens na kumaliza na ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Hivyo, pamoja na ugeni, ASEC ni timu iliyoonyesha upinzani mkubwa na beki wa Kitanzania, Violeth anapaswa kuwa makini dhidi ya kiungo mshambuliaji Habibou Ouedraogo anayeonekana kuwa hatari akifunga mabao mawili kupitia mechi tatu alizocheza.
Ukiachana na mechi hiyo ya nusu fainali ya kwanza ambayo Watanzania wanatarajiwa kuliamsha kupitia Masar, pambano jingine tamu la watetezi Mazembe na AS FAR ni kama fainali kutokana na ugumu na ushindani mkubwa wa vikosi hivyo.
Ni kama mechi ya kisasi baada ya msimu uliopita kukutana katika fainali na Mazembe ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutawazwa mabingwa mbele ya Waarabu hao waliokuwa wenyeji. Washindi wa mechi za leo watakutana fainali itakayopigwa wikiendi, huku rekodi zikionyesha katika misimu minne iliyopita tangu 2021 ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyotwaa mara mbili, huku FAR Rabat na TP Mazembe zikitwaa mara moja-moja.
