TAASISI ya The Same Qualities Foundation (SQF), waandaaji wa SQF Zanzibar Marathon, imetangaza kuanza rasmi kambi ya upasuaji kwa watoto wenye ugonjwa wa midomo wazi (Sungura) hadi Desemba 19, 2025 kabla ya kilele cha mbio za kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo.
Kambi hiyo imeanza Novemba 15, 2025 na inaendeshwa katika Hospitali ya Mkoa, Lumumba kisiwani hapa huku kilele chake kukiwa na SQF Zanzibar Marathon, Desemba 21, 2025 mjini Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, Mwenyekiti wa Waandaji wa Mbio za Barabarani, Joseph Katembo, amesema tangu kuanzishwa kwa mbio hizo wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji watoto 2,543 kati yao 240 wanatoka kisiwani hapa.
Amesema, wameamua mbio hizo kuzifanyia hapa kwa sababu ni miongoni mwa eneo lenye idadi kubwa ya watoto wenye ugonjwa huo.
Vilevile, amesema watoto wenye ugonjwa huo wamekuwa wakitelekezwa, kufichwa na kunyimwa fursa ya kupata elimu, ndiyo maana wanataka kusaidia kuondoa hali hiyo.
“Kwa miaka mingi mbio hizi zimekuwa zikifanyika Arusha lakini mwaka huu tumeamua kufanyia kisiwani hapa kwa sababu watoto wenye ugonjwa huo ni wengi na wanahitaji matibabu,” amesema Katembo.
Naye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Zanzibar, Muhidin Yassin amewaomba wananchi kuchagia hata kwa ambao hawatashiriki mbio hizo.
Muhidin amesema, Watanzania wajitokeze kuchangia na kushiriki mbio hizo ili kuwasaidia watoto hao kufanyiwa upasuaji na sio kuwaweka ndani kukosa haki ikiwemo elimu.
Naye, mratibu wa mbio hizo, Amry Massare amesema mbio hizo ni muhimu kwani zinakwenda kutoa huduma kwa watoto wa midomo wazi.
Amesema, mbio hizo ni kilomita tano, 10 na 21 ambapo medali za washindi zitatolewa kutokana na mchango wao ushiriki kwa ajili ya jamii na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha mbio hizo.
