Abiria wanaotumia usafiri wa anga waongezeka, sababu zatajwa

Tanga. Kukua kwa sekta ya utalii na miradi mikubwa ya uwekezaji ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuongezeka kwa abiria wanaotumia usafiri wa anga kwa asilimia 16 kutoka mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi ametoa taarifa hiyo leo Novemba 18, 2025 wakati wa kikao cha 58 cha uwezeshaji wa usafiri wa anga kilichofanyika jijini Tanga.

Amesema mwaka 2020, viwanja vya ndege Tanzania vilipokea abiria milioni mbili, kwa mwaka wakati mwaka 2022 idadi ya abiria ilifikia milioni nne ambapo mwaka huu wamepokewa abiria milioni 7.4.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa anga Tanzania (TCAA),Salim Msangi

“Mwaka 2022, abiria walipungua kwa sababu ya mlipuko wa Uviko-19 lakini mwaka huu, ongezeko limefikia asilimia 16 na hadi mwakani tunatarajia kuwahudumia abiria milioni 8.4,” amesema Msangi.

Amesema kikao hicho kinawakutanisha wadau wa usafiri wa anga wakiwamo watoa huduma ambao watajadili namna ya kuboresha huduma ili ziwe za kuvutia abiria pamoja na kutembelea viwanja vya ndege, na kushauri mamlaka husika namna ya kuboresha miundombinu ya viwanja hivyo.

“Kwa hapa Tanga, pamoja na kujadiliana mikakati ya uboreshaji huduma zetu pia, kwa kipindi cha situ tatu tutakazokuwa hapa tutatembelea uwanja wa ndege wa Tanga kukagua huduma zinazotolewa na kushauri nini kifanyike katika kuboresha,” amesema Msangi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanyia ukarabati mkubwa uwanja wa ndege wa Tanga ikiwa ni sehemu ya kurahisisha shughuli za uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt Batilda Burian

“Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege utakaohimili abiria wanaokuja kwa shughuli za uwekezaji na vivutio vya utalii zikiwemo hifadhi za Taifa za Saadan na Mkomazi.

Ametaja miradi mikubwa inayoendelea mkoani Tanga kuwa ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani, bandari ya Tanga kupokea meli kubwa, viwanda vya saruji na  bomba la gesi linalotarajiwa kujengwa.

“Bandari ya Tanga imeongeza uwezo wa kupokea meli kutoka 18 kwa mwezi hadi kufikia meli 58..mwezi uliopita tulipokea meli yenye ukubwa wa tani 33,000 ambapo walioajiliwa kufanya kazi walifikia vijana 16,000″amesema Balozi Burian.

Amewaagiza wadau wa usafiri wa anga nchini kuongeza mbinu za kuwahamasisha Watanzania kutumia usafiri wa ndege na kuachana na kasumba iliyojengeka kuwa kupanda ndege ni anasa.