ACT-Wazalendo wapinga uteuzi wajumbe tume ya uchunguzi

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kuikataa Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuatia, kikisema kuwa tume hiyo haina sifa ya kuleta ukweli, uwazi wala haki kwa waathirika.

Mapema, leo Jumanne, Novemba 18, 2025, Rais Samia ametangaza majina ya wajumbe saba wa tume hiyo akiwemo Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma; Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Mwanadiplomasia Balozi Radhia Msuya; pamoja na Balozi Paul Meela.

Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Ally Mwema; Balozi David Kapya; na Waziri wa zamani wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.

Kwa mujibu wa Ikulu, hatua ya kuteua tume hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia aliyoitoa Novemba 14, 2025 wakati akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma, alipoeleza kusikitishwa kwake na matukio hayo na kuahidi kuyachunguza.

Matukio ya Oktoba 29 na siku zilizofuata yalitokea katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Geita, Arusha, Mara na Ruvuma na yalisababisha vifo vya raia, majeruhi wengi, uharibifu wa mali za watu binafsi na miundombinu ya umma.

Hata hivyo, ACT Wazalendo imesema tume hiyo ni “dhihaka kwa waliopoteza maisha, majeruhi na familia zilizofiwa,” ikieleza kuwa baadhi ya wajumbe ni watu wanaotoka katika taasisi ambazo zinapaswa kuchunguzwa badala ya kupewa jukumu la kuchunguza.

Kupitia taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Ado Shaibu imeeleza kuwa hataweza kuipa uhalali tume hiyo.

“Hatuwezi kuipa tume hii uhalali kwa sababu imeundwa na watu ambao taasisi zao zinadaiwa kuhusika moja kwa moja katika tukio lenyewe. Huu si utaratibu wa kutafuta ukweli, huu ni utaratibu wa kulinda wahusika,” ameeleza Ado kupitia taarifa hiyo na kuongeza kuwa: “Hakuna familia iliyoathirika, hakuna mwananchi yeyote mwenye kiu ya haki atakayeiambia tume hii ukweli wake halisi. Hii si tume huru na kwa mantiki hiyo haiwezi kuleta haki,”.

Chama hicho kimesema tume ya namna hiyo si huru na ni jaribio la kuficha makosa na kuwalinda waliohusika katika unyanyasaji huo.

ACT Wazalendo kimetangaza kuwa hakitashiriki kwa namna yoyote katika kazi ya tume hiyo, hakitatoa ushahidi wala ushirikiano, kikisisitiza kuwa chombo hicho “kitategemea maagizo ya serikali” na hakiwezi kuaminika kuleta haki.

Badala yake, chama hicho kinataka kuundwa kwa tume huru ya Kimataifa, itakayojumuisha wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika, taasisi za kimataifa za haki za binadamu au vyombo vingine vinavyoaminika kimataifa.

Kwa mujibu wa chama hicho, ni tume ya aina hiyo pekee inayoweza kuleta ukweli, kuwapa haki wasthirika na kuzuia matukio kama hayo kutorudi tena.

“Tunaomba jumuiya ya kimataifa isimame na wananchi wa Tanzania. Uchunguzi huru wa kimataifa si ombi la kisiasa, ni hitaji la msingi la haki. Taifa letu linahitaji ukweli ili liweze kusonga mbele,” ameeleza Ado.