Shinyanga. Mwendesha bodaboda, Stefano Maziku maarufu kama Doto (25), mkazi wa kitongoji cha Igwesa Kijiji cha Iboja kilichopo Wilaya ya Kipolisi Ushetu mkoani Shinyanga, amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Novemba 18, 2025 na jeshi hilo linawasaka waliotekeleza kitendo hicho cha uhalifu.
Kamanda Magomi amesema tukio hilo limetokea Novemba 16, 2025 na mwili wa Doto ulikutwa na jeraha lililoashiria kukatwa na kitu kinachodhaniwa kuwa na ncha kali shingoni, kisha kutobolewa jicho la upande wa kushoto.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali kwani baada ya wahalifu kutekeleza tukio hilo walitoweka na pikipiki ya marehemu yenye namba za usajili MC 799 FCV na kutokomea kusikojulikana.
Aidha, Kamanda Magomi amewataka maofisa usafirishaji mkoani humo kuwa makini na watu wasiowajua wanaowakodisha hususani nyakati za usiku kwani wengi huwa na nia ovu.
“Kwanza, tunakemea kitendo kama hiki maana kila binadamu ana haki ya kuishi, niwaombe wananchi wote wakiwemo wa Ushetu, tushirikiane kuwabaini watu hawa waliotekeleza kitendo hiki kibaya,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Katibu wa kituo cha bodaboda Iboja, Naftali Zabron amesema siku moja kabla ya tukio Novemba 15, 2025, Doto alifanya kazi zake bila tatizo lolote.
Amesema siku hiyo mpaka saa tatu usiku alimuona marehemu enzi za uhai wake akiwa anaendesha pikipiki huku akimpakia mdogo wake na baada ya hapo wakaagana, ndipo asubuhi walipopata taarifa za kuuawa kwake.
“Siku moja kabla ya tukio, huyu kijana alifanya kazi vizuri tu na mpaka saa tatu usiku tulimuona akiwa amempakia mdogo wake, baada ya hapo sikumuona tena mpaka napigiwa simu ya tukio,” amesema na kuongeza:
“Tulipofika eneo la tukio ilikuwa ni saa mbili asubuhi na tulikuta damu bado mbichi kabisa, ikiashiria kwamba mwenzetu ameuawa si muda mrefu sana, labda saa 11 alfajiri kuja saa 12 hivi, inauma sana.”
