Kocha Mreno aweka mkakati Yanga, mastaa sita wakitajwa

YANGA imetua Kisiwani Zanzibar jana tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuwa mwenyeji wa AS FAR Rabat ya Moroco kwenye mechi ya kwanza hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mabingwa hao wa Tanzania wanaonolewa na Kocha Mreno, Pedro Goncalves kama wanataka kufanya vizuri lazima wawatulize mastaa sita wa wapinzani wao huku mwenyewe akitaja mambo mawili.

Yanga inaanzia nyumbani, mechi ikipigwa Novemba 22, mwaka huu Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kila timu ikitaka kuanza vyema kampeni hiyo ya Kundi B ambalo pia lina Al Ahly ya Misri na JS Kabylie kutoka Algeria.

Wakati kikosi cha Yanga kikielekea Zanzibar, Kocha Pedro alisema licha ya kubaki na siku chache, watajaribu kuweka nguvu kutengeneza utayari wa wachezaji kiakili na mbinu kulingana na ubora wanaoujua wa wapinzani wao.

“Tuna siku chache kweli, lakini tuna wachezaji wenye uzoefu, naamini hawa wengine watafika kwa wakati wakiwa salama, tutawatengeneza kisaikolojia na kuongeza mbinu kadiri muda utakavyotosha ili waweze kukabiliana na wapinzani wetu,” alisema Goncalves.

Wachezaji ambao wamekosekana katika msafara huo uliondoka jana ni wale waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa ukiachana na wale waliokuwa Taifa Stars ambao tayari wamerudi ni Celestine Ecua na Lassine Kouma (Chad), Prince Dube (Zimbabwe), Duke Abuya (Kenya) na Djigui Diarra (Mali).

Wakati Goncalves akiwa na hesabu hizo, katika kikosi cha AS FAR Rabat, kuna mastaa sita wanaoonekana kuwa hatari zaidi ambao Yanga inapaswa kuwachunga. Mwanaspoti linakuchambulia.

MRE 01

Mtihani wa kwanza kwa Yanga upo hapa, ni lazima watafute dawa wa kuipangua safu ya ulinzi inayoundwa na mabeki wa kati Marouane Louadni anayecheza sambamba na Yunis Abdelhamid.

Achana na Louadni aliyecheza mechi saba hadi sasa, kuna huyu Abdelhamid ambaye FAR Rabat imemsajili kutoka Saint-etienne inayoshiriki Ligue 1, Ufaransa ambaye amecheza mechi tano tu akiwa na ubora mkubwa wa kupambana na mipira ya juu na hesabu nzuri katika kukabiliana na washambuliaji.

Kocha Alexander Santos akimpumzisha mmoja kati ya hao, anamtumia Fallou Mendy raia wa Senegal ambaye licha ya kucheza mechi chache lakini amefunga bao la kichwa kutokana na mipira iliyokufa.

MRE 02
MRE 02

Mtu mwingine hatari kwenye ukuta huo ni beki wa kushoto, To Carneiro ambaye kocha wa Yanga Goncalves anamjua vizuri kwani ndiye beki wake alipokuwa anaifundisha timu ya taifa ya Angola.

Carneiro anajua kukaba na kupandisha mashambulizi, pia anafunga kwa mashuti makali. Msimu huu amecheza jumla ya mechi tano za ligi, akipumzishwa tu anapotumiwa Jamal Ech Chamakh ambaye amecheza mechi tatu msimu huu.

Ukuta huu licha ya ubora wake unaweza kufanya makosa na hadi sasa katika mechi nane za ligi ya ndani umeruhusu mabao matano na mawili kwenye mechi mbili za ugenini hatua ya za mtoano Ligi ya Mabingwa Afrika.

Juzi Carneiro alikuwa akipambana na Lionel Messi wa Argentina katika mechi ya kirafiki iliyomalizika kwa Angola kufungwa 2-0.

MRE 03

Eneo la kiungo mtu hatari wa kwanza ni nahodha huyu anayecheza eneo la ukabaji, akiwa amecheza mechi zote nane za ligi, ndiye masta plani wa mambo yote hatari ya AS FAR Rabat akijua kukaba kwa hesabu na kupiga pasi hatari.

Yanga kama wanataka kufanya vizuri hawatakiwi kumruhusu Hrimat kucheza kwa uhuru wake, kitu kibaya zaidi ndiye mfungaji bora kwenye ligi ya kwao akiwa amefunga mabao matano na asisti moja.

Kocha Goncalves anamjua vizuri Hrimat kwani katika michuano ya CHAN 2024, walikutana Morocco ilipoichapa Angola mabao 2-0 pale nchini Kenya huku kiungo huyo akitoa asisti moja.

MRE 04

Mwingine ni huyu Anas Bach aliyecheza mechi sita msimu huu, anajua sana kuutafuta mpira lakini pia ana kasi ya kupandisha mashambulizi, ameshafunga bao moja na kutoa asisti moja.

MRE 05

Msimu wa 2022-2023 katika Ligi Kuu ya Morocco, Reda Slim alikuwa mchezaji bora, baada ya hapo akasajiliwa na Al Ahly ya Misri, kisha akaja hapa Tanzania kucheza dhidi ya Simba kwenye mashindano ya African Football League (AFL) na akawafunga wekundu hao wakilazimisha sare ya bao 1-1.

Reda amerudi klabuni kwake baada ya kuchemsha pale Ahly na ameanza moto wake akiwa ameshacheza mechi saba hadi  sasa za ligi ya kwao, huyu ni kiungo hatari mshambuliaji akiwa karibu na uso wa goli, viungo na mabeki wa Yanga wanatakiwa kumnyima utulivu wa kufanya uamuzi.

MRE 06

Huyu ni mshambuliaji wao hatari, ana kasi na kujua kulichagua goli kwenye kufunga, mabeki wa Yanga wanatakiwa kujipanga hapa kwani jamaa anaweza kufunga kwa kichwa pia anapiga kwa nguvu akitumia miguu yote.

Fahli sio aina ya mshambuliaji ambaye anahitaji nafasi mbili kufunga, kama yakitokea makosa kwa Yanga kumsahau hata kwa nafasi moja anaweza kuwaliza, msimu huu ndiye mfungaji wao namba mbili nyuma ya Hrimati akifunga mabao manne na asisti moja.

Kocha Santos akimpumzisha Fahli basi anampa nafasi Mouchcine Bouriga kucheza nafasi hiyo ambaye sio mbovu sana lakini anahitaji kuchungwa kama atapewa nafasi.