Na. Mwandishi Wetu-DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Willium Lukuvi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumrudisha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.
Mhe. Lukuvi ametoa shukrani hizo leo tarehe 18 Novemba, 2025 Jijini Dodoma wakati wa zoezi la kuwapokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo katika Ofisi za Waziri Mkuu Ngome.
“Kwanza ninampongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi wa kupata kura nyingi, lakini pia ninamshukuru kwa kuniamini na kunirudisha tena kuhudumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni mara ya nne kuhudumu ndani ya ofisi hii” ameeleza Mhe. Lukuvi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi amewapongeza kwa uteuzi huo na kusema kuwa ofisi yake ipo tayari kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na juhudi ili kuweza kutimiza malengo ya Mhe. Rais.
“Nawapongeza kwa kuaminiwa na kuteuliwa tena na Mhe. Rais, tupo tayari kufanya kazi nanyi kwa bidii, uaminifu na juhudi zote ili kuweza kutimiza malengo ya serikali kwa ufanisi” amebainisha Dkt. Yonazi.





