Mahakama yaridhia Jamhuri kuongeza walalamikaji 100 kesi ya ‘Dk Manguruwe’

Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe umedai umebaini walalamikaji zaidi 100 hawajajumuishwa katika hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo pamoja na mwenzake.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iwape muda ili waweze kuwaongeza walalamikaji hao katika hati ya mashtaka kabla ya kuwasomea hoja za awali (PH).

Ombi hilo limekubaliwa na Mahakama hiyo na sasa hati ya mashtaka ya kesi hiyo itasomwa upya, Alhamisi Novemba 20, 2025.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu kama Dk Manguruwe akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Leo, Jumanne Novemba 18, 2025 Wakili wa Serikali, Titus Aron, ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusomwa hoja za awali(PH).

“Kesi imeitwa leo kwa ajili ya Jamhuri kuwasomea hoja za awali washtakiwa hawa, lakini kwa bahati mbaya jana jioni wakati napitia jalada hili, nilibaini zaidi ya walalamikaji 100 walikuwa hawajajumuishwa kwenye hati ya mashtaka” amedai Wakili Aron na kuongeza.

“Hivyo, jana ileile nilianza kuwajumuisha katika hati ya mashtaka lakini mpaka leo bado sijamaliza na tukumbuke walalamikaji hao ndio mashahidi katika kesi hii, hivyo tunaiomba Mahakama itupe muda ili tuweze kukamilisha na baada ya hapa, tutafanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na kuwasomea upya hati hiyo na kisha kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo (PH),” amesema Aron.

Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kushindwa kuendelea na usomwaji wa hoja za awali (PH) katika kipindi cha siku mbili mfululizo, kwani Novemba 17, 2025 kesi hiyo ilipagwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa PH, lakini upande wa mashtaka ulidai kuwa bado haujakamilisha kupandisha nyaraka hizo kwenye mtandao wa Mahakama na kuiomba iahirishe hadi Novemba 18 (ambayo ni leo).

Wakili Aron baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi Shindi Mrutu alidai kuwa kilichozungumzwa na upande wa mashtaka ni kurudisha nyuma kesi hiyo.

“Mheshimiwa hakimu, hati ya mashtaka iliyopo mbele ya Mahakama ni ya Novemba 5, 2024 na mpaka sasa ni zaidi ya mwaka umefika na wiki iliyopita walisema upelelezi umekamilika na wakatupatia nyaraka kama sheria inavyotaka na kilichobaki ni kutusomea PH, sasa leo hii taarifa iliyotolewa na Jamhuri ni kitu kigeni kwetu, walikuwa wapi muda wote? Tunaomba tuongozwe na sheria,” amesema wakili Mrutu.

Mrutu baada ya kutoa hoja hiyo, Hakimu Nyaki, amehoji upande wa mashtaka kama wanaweza kuwafungulia kesi nyingine ili hiyo iliyopo mahakamani hapo iweze kuendelea na usikilizwaji.

Akijibu swali hilo, wakili Aron amedai maelezo ya walalamikaji hao tayari yapo kwenye rekodi za mashahidi ambao kutajwa wakati wa usomwaji wa PH, hivyo hawawezi kufungua kesi nyingine, badala yake watafanya mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kuwaongeza walalamikaji hao katika kesi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu kama Dk Manguruwe akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Hakimu Nyaki amesema tayari ameshaona baadhi ya nyaraka za zilizosajiliwa na Jamhuri kwenye mtandao wa Mahakama ambazo zitatumika wakati wa usomwaji wa PH, huku akiuliza upande wa utetezi kama na wao wameziona.

Hata hivyo, upande wa utetezi walidai kuwa wameona za mashahidi 10 tu.

Ajibu hoja hiyo, wakili Aron amedai nyaraka walizosajili kwenye mfumo ni nyingi na sio za mashahidi 10 pekee, hivyo aliwashauri mawakili wa utetezi waingie kwenye mfumo ili waweze kupakua nyaraka hizo kwa ajili ya kuzitumia katika kesi hiyo.

“Nyaraka zilizosajiliwa na Jamhuri katika mtandao wa Mahakama ni nyingi, sidhani kama ni za mashahidi kumi…hapa nimeona zipo batch 3 (makundi matatu) kundi la kwanza lina kurasa 150, kundi la pili lina kurasa 200 na kundi la tatu bado halijafunguka, hivyo upande wa utetezi mnatakiwa mpewe ili mjiandae kwa PH” amesema Hakimu Nyaki.

Baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, 2025 ambapo Jamhuri watawasomea upya hati ya mashtaka na hoja za awali.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28; mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi,2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo.

Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa  Mkaguzi wake waliendesha  biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi  tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi cha Sh92.2milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashtaka 9 ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya peke yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.

Mkondya anaendelea kusalia rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili hayana dhamana huku John akiwa nje kwa dhamana kutokana na kutokuwa na mashtaka ya kutakatisha fedha.