WINGA wa Geita Gold, Yusuph Mhilu amesema anaamini msimu huu ni wa kufa ama kupona kwa timu hiyo katika safari yao ya kurejea Ligi Kuu Bara, huku akisistiza hakuna visingizio.
Mhilu amedumu na timu hiyo kwa msimu wa tatu sasa baada ya kujiunga nayo 2023-2024 akitokea Simba, kisha akashuka nayo daraja na msimu uliopita akakipiga Ligi ya Championship.
Msimu uliopita, timu hiyo iliishia hatua ya mtoano baada ya kufungwa mabao 2-0 na Stand United ya Shinyanga, ndoto ya kurudi Ligi Kuu ikayeyuka.
Kwa msimu huu, Geita Gold imeanza vizuri Ligi ya Championship ikishika usukani baada ya kuvuna alama 13 katika mechi tano, ikishinda nne na sare moja, huku ikifunga mabao 11 na kuruhusu mawili.
Mhilu aliliambia Mwanaspoti kwamba, umekuwa msimu mzuri kwao kama klabu kwakuwa mipango yao inakwenda vyema mpaka sasa, jambo ambalo linawapa matumaini ya kumaliza katika malengo yao.
“Umekua msimu mzuri kwa sababu tumeanza vizuri na tuna matumaini ya kutimiza malengo yetu japokuwa utakuwa msimu wa ushindani kutoka na ubora wa timu tunazoshindana nazo,” alisema Mhilu.
Alisema matarajio yake ni kuipandisha daraja timu hiyo na kuirejesha Ligi Kuu Bara, huku akijiwekea malengo ya kuwa mfungaji bora baada ya msimu uliopita kumaliza na mabao 10 na assisti moja.
“Matarajio yangu ya kwanza ni kupandisha timu, pili ni kufanya vizuri ili niwe mchezeji bora au mfangaji bora wa ligi ili nipandishe thamani yangu kwenye vipindi vya usajili, mpaka sasa nimefunga bao moja.
“Mipango ya timu msimu huu ni kushika nafasi mbili za juu na kupanda daraja yaani kurudi Ligi Kuu,” alisema Mhilu.