Mawaziri wataja uzalendo, ubunifu kukabiliana na ukosefu fedha

Chamwino. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Serikali kujitegemea katika miradi kutokana na hofu ya kukosa mikopo, imeamsha ari ya mawaziri ambao wameahidi kuwa wanakwenda kupambana.

Rais Samia amesema kuna wasiwasi kuhusu kukubalika kwa Serikali katika mikopo kwa baadhi ya mataifa kutokana na alichosema machafuko yaliyotokea kwamba yameiweka Tanzania katika sifa mbaya, hivyo akawataka mawaziri kusimama na kutafuta fedha za ndani ili waweze kutekeleza miradi.

Kufuatia kauli hiyo, Waziri wa Viwanda, Judith Kapinga amesema kauli ya Rais imewapa angalizo na kwamba jambo la msingi kabisa ni wao kwenda kutumia akili na maarifa ili kutimiza malengo yanayotakiwa.

Kapinga amesema ndani ya wizara hiyo zinahitajika fedha nyingi kwa ajili ya kujenga na kufufua viwanda vilivyokufa ili wakatoe ajira milioni nane zilizoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo kukosekana kwa fedha ni wazi kuwa wanahitaji kutumia akili nyingi na maarifa ya hali ya juu.

“Wizara ya Viwanda ni injini ya uchumi. Zile ajira milioni nane kwenye Ilani ya CCM zinapaswa kuzalishwa na viwanda, kwa sababu hiyo ni lazima tuendelee kukimbia kwa kutumia akili na maarifa yetu ili tufanikiwe; hapa akili zaidi itatumika ili wananchi watuelewe,” amesema Kapinga.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema miradi mingi inayotekelezwa katika wizara yao inahitaji fedha za kutosha ambazo sasa huenda zisipatikane kama alivyosema kiongozi wa nchi, lakini Taifa linahitaji kufunguliwa kwa namna yoyote.

Kasekenya amesema kauli ya Rais kwamba hataki maneno bali anataka matokeo ni agizo zito ambalo kila anayelitafsiri kwa mapana anahitaji kutumia muda wake mwingi kujenga mawazo ya kulisaidia Taifa.

“Ametwambia hapo kuwa hataki maneno na sababu, bali anataka matokeo. Lakini mmesikia amesema kuwa miaka mitano siyo mingi, ni lazima tukimbie. Nami nasema tuko tayari kwa ajili hiyo ili tutumie akili zetu na maarifa katika kukwepa sababu kwenye ukamilishwaji wa miradi,” amesema Kasekenya.

Akizungumzia kauli hiyo na maagizo ya kuwataka mawaziri wakimbie, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema imani aliyopewa na Rais ni kubwa, hivyo yaliyoagizwa lazima akayatimize kwa nguvu na maarifa zaidi ili Watanzania waendelee kupata maji.

Kwa mujibu wa Aweso, milango ya kutekeleza miradi itafunguka na wanyonge wataendelea kupata haki yao kama ilivyotarajiwa, hata kama kutatokea changamoto ya namna yoyote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Regina Ndege, amesema tafsiri ya kazi na utu ndiyo kipimo cha utumishi katika kipindi hiki bila kuangalia nyuma, kwani kiongozi wa nchi akisema hakuna namna, kinachotakiwa ni kupanga namna ya kumsaidia.

Regina amesema malengo ya Rais yatatimia ikiwa mawaziri, manaibu waziri na makatibu wakuu watafanya kazi kwa ushirikiano kwa lengo la kuwasaidia wanyonge bila kutanguliza masilahi binafsi, na kwamba kila mmoja anatakiwa kubeba mzigo huo.