Dar es Salaam. Itakuwa ni karibu siku 20 tangu huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi kukosekana katika njia ya Mbagala na Kimara ikiwa ni baada ya kuharibika kwa miundombinu yake katika vurugu za maandamano ya siku ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Kufuatia kukosekana kwa usafiri huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameziagiza kampuni ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Udart) pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali zilizo chini ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha ifikapo Novemba 20, 2025, huduma za usafiri huo zinarejea katika Barabara ya Mbagala kuelekea katikati ya jiji.
Kwa tafsiri hiyo, Mbagala itaanza mapema Alhamisi huku njia ya Kimara mkuu huyo wa mkoa akiwa hajaweka wazi tarehe ya kurejea kwa huduma hiyo ingawa ameahidi hivi karibuni.
Chalamila ametoa agizo hilo leo Jumanne, Novemba 18, 2025, wakati alipotembelea vituo vya mabasi ya mwendokasi katika njia ya Mbagala pamoja na kukagua miundombinu iliyoharibika katika siku hiyo.
Kwa upande wa Mbagala, Serikali kupitia mkuu huyo wa mkoa ilitangaza kusitisha usafiri wa mabasi hayo huku akiwataka waliokuwa watumiaji kutafuta njia mbadala za usafiri wakati ambao unafanyika utaratibu wa kurudisha hali kama ilivyokuwa awali.
Ikumbukwe mwendokasi Mbagala ilianza huduma Oktoba 12, 2025 ambapo ilifanya kazi kwa takribani siku 17 hadi Oktoba 29, 2025 ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali ulihusisha mabasi 250 ya Kampuji ya Mofat.
Akieleza hii, leo Chalamila amesema kwa sasa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya umma na mali za watu binafsi, sambamba na kuwatambua walioathirika kiafya au kupoteza mali.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuweka kando hasira na kuendelea kulijenga Taifa kwa pamoja.
“Leo ni Novemba 18 nawaelekeza taasisi zote za Serikali zinazohusika kwa pamoja wahakikishe Novemba 20, 2025 Alhamisi saambili asubuhi au hata kabla mabasi yote yanaingia kwenye barabara,” ameagiza.
Kuhusu njia ya mwendokasi inayotoka Gerezani kuelekea Kimara, Chalamila amesema Serikali inaharakisha urejesho wa huduma ili usafiri urejee katika hali ya kawaida haraka iwezekanavyo.
