NACTVET yaagiza vyuo kufuata utaratibu

Na Mwandishi Wetu Dodoma

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limesema kuwa liliratibu udahili wa wanafunzi kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kuanzia tarehe 28 Mei 2025 na kuhitimishwa Oktoba 28 ,2025.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma Katibu Mtendaji wa NACTVET Dkt.Mwajuma Lingwanda amesema udahili wa Wanafunzi kwa Kozi za Afya na Sayansi Shirikishi kwa Tanzania Bara yalifanyika kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (CAS) na kwa upande wa Zanzibar maombi yalifanyika moja kwa moja vyuoni.

Amesema jumla ya waombaji 49,148 walituma maombi ya kujiunga na vyuo katika programu mbalimbali ambapo Waombaji 39,553 sawa na asilimia 80 ya waombaji wote walichaguliwa ambapo kati yao wanawake ni 20,131 sawa na asilimia 51 na wanaume ni 19,422 sawa na asilimia 49.

Dkt.Mwajuma Maombi kwa kozi zisizo za afya yalitumwa moja kwa moja vyuoni na kisha vyuo viliwasilisha majina ya wanafunzi waliochaguliwa NACTVET kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.

Aidha jumla ya wanafunzi 108,109 waliochaguliwa na vyuo waliwasilishwa NACTVET kwa uhakiki wa sifa zao ambapo kati yao 106,022 sawa na asilimia 98 ya waombaji wote walikua na sifa za kujiunga na kozi au programu walizoomba.

Hata hivyo amesema changamoto zilizojitokeza katika udahili baadhi ya vyuo kuchagua waombaji wasio na sifa stahiki kwa vyuo visivyotumia Mfumo wa Udahili wa Pamoja(CAS) pamoja na Vyuo kuwasilisha maombi ya udahili kwa niaba ya waombaji bila ridhaa yao, au kutumia namba za simu ambazo si za waombaji husika

Dkt Mwajuma amesema hatua zilizochukuliwa na Baraza kutoa fursa ya marekebisho kwa waombaji kuomba programu wanazokidhi sifa stahiki ambapo fursa hiyo ilikuwa wazi hadi Novemba 30,2025 na kuwataka wanafunzi juu ya umakini katika utunzaji na utoaji wa taarifa zao.

Aidha amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitangaza kufunguliwa kwa vyuo vyote nchini kwa awamu mbili kama ifuatavyo kwa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza watawasili vyuoni kuanzia tarehe 17 Novemba, 2025 na wanafunzi wanaoendelea na masomo watawasili vyuoni kuanzia Novemba 24 , 2025

Dkt.Mwajuma amesema mambo ya muhimu ya kuzingatia kwa vyuo na wanafunzi waliodahiliwa kwa mwaka wa masomo 205/2026 na wale wanaoendelea na masomo Vyuo vinasisitizwa kuwasajili wanafunzi wote waliochaguliwa na kufika vyuoni

ndani ya muda uliopangwa Novemba 17 2025 hadi Desemba 12,2025, Vyuo kutopokea wanafunzi ambao hawakuchaguliwa kwenye vyuo husika pamoja na Vyuo hivyo kutosajili mwanafunzi ambae hajafika chuoni.

Baraza linawataka Wanafunzi wanatakiwa kuwasili katika vyuo walivyochaguliwa na kujisajili ndani ya muda uliopangwa na baada ya mwanafunzi kusajiliwa na chuo chake, aingie katika tovuti ya NACTVET www.nactvet.go.tz kuthibitisha usajili wake na kuhakiki taarifa zake kwa kubofya“link” inayosomeka “student’s information verification” na iwapo mwanafunzi atathibitisha kutokuwepo taarifa zake sahihi, atoe taarifa chuoni kwake na pia NACTVET kupitia mawasiliano ya Baraza

Wanafunzi wanaoendelea na masomo wanatakiwa kuhakikisha wamesajiliwa kwenye mfumo wa NACTVET na taarifa zao ikiwemo chuo, program na matokeo ya muhula husika ni sahihi na endapo taarifa zao si sahihi wawasiliane na vyuo vyao pamoja na kutoa taarifa NACTVET.

Baraza limeandaa dawati maalum kwa ajili ya kutoa usaidizi kwa wanafunzi na vyuo katika kipindi chote cha usajili wa wanafunzi vyuoni.

Baadhi ya watumishi wa NACTVET  katika mkutano na waandishi wa habari.