Dodoma. Nani kamuua mchekeshaji maarufu nchini Tanzania, Emmanuel Mathias, maarufu MC Pilipili pengine ndio swali linalogonga vichwa vya wengi kwa sasa. Nani amehusika kwenye mauaji yake na kwa nini amefikia hatua hiyo.
Swali hilo linatokana na taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuthibitisha kwamba, kifo cha MC Pilipili kimetokana na kupigwa.
leo Novemba 18,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gallus Hyela amesema kuwa, wameshirikiana na madaktari kuufanyia uchunguzi mwili wa MC Pilipili na kubaini kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida, hivyo wameanza uchunguzi mara moja kubaini waliohusika.
“Ni kweli, tumeshirikiana na wataalamu ambao ni madaktari, mwili ule tumebaini ulikuwa na alama zinazoonyesha kulikuwa na shida ambayo ni kipigo, maana alama zile hazikuwa za kawaida, hivyo tumeanzisha uchunguzi mara moja kujua nini kilitokea na tungeomba yeyote mwenye taarifa za siri juu ya jambo hilo atupatie,” amesema Hyela.
Mwili wa MC Pilipili ulipokelewa siku ya Jumapili ya Novemba 16,2025 saa 11 jioni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo inaelezwa kuwa ulipelekwa na wasamaria wema.
Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Ernest Ibenzi alithibitisha kuwa walipokea mwili wa MC Pilipili ambapo waligundua kuwa tayari alikuwa amepoteza maisha na walioupeleka hapo walitajwa kuwa ni wasamaria wema.
