Muheza. Wakulima nchini wanatarajia kuanza uzalishaji wa mazao kwa tija kufuatia Wizara ya Kilimo kuandaa programu itakayowawezesha kupata taarifa sahihi kuhusu rutuba iliyomo mashambani mwao pamoja na mbolea inayopaswa kutumiwa.
Taarifa hizo zitaanza kutolewa na Serikali kidijitali baada ya wataalamu 45 wa utafiti wa udongo na mbolea kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, walio katika mafunzo ya wiki moja katika kituo kikuu cha utafiti wa udongo cha Mlingano, Wilayani Muheza mkoani Tanga kutoa taarifa ya pamoja ya itifaki ya udongo.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango (DLUP) kutoka Wizara ya Kilimo, Juma Mdeke wakati akifungua mafunzo ya siku sita ya wataalamu hao kutoka taasisi za utafiti wa udongo na mbolea zilizo chini ya wizara hiyo.
Amesema ripoti ya itifaki ya pamoja ya utafiti wa udongo ikikamilika itakuwa imefanyika kwa mara ya pili katika historia ya Tanzania baada ya ile iliyotolewa mwaka 1984.
“Kazi hii ni muhimu kufanyika kwa sababu mara ya mwisho ilifanyika mwaka 1984 kupata ramani ya nchi nzima ya udongo lakini kwa kipimo cha 1 kwa milioni mbili na sasa hivi sisi tunapima udongo kwa skeli ya 1/50,000,” amesema Mdeke.
Ameongeza kuwa: “Wataalamu hawa waliopo katika mafunzo haya wanafundishwa njia sahihi ya kutafiti sampuli za udongo na kisha kutayarisha ripoti ya itifaki ya udongo yenye kukubalika kimataifa…itasaidia kwa kiasi kikubwa kwa wakulima kuwa na taarifa sahihi kuhusu aina gani ya mazao yatakayostawi katika mashamba yao.”
Mkurugenzi wa utafiti na ubunifu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Deusdedit Mbazigwa amesema watafiti hao watapewa mafunzo ya tafsiri ya pamoja ya maabara ya sampuli za udongo zilizokusanywa kutoka maabara mbalimbali za udongo nchini.
“Programu hii itawawezesha wakulima nchini kujua udongo uliopo mashambani una rutuba kiasi gani na mimea gani inastahili na kama ni mbolea ya aina na kiwango kipi,” amesema Mbazigwa.
Amesema kupitia programu hiyo, Serikali itakuwa inajua mahitaji ya mimea na aina ya mbolea iliyopo ambapo itafanyika kwa kutumia protokali tofauti za udongo.
Amezitaja taasisi zinazoshiriki katika programu hiyo ijulikanayo kama TFSRP kuwa ni Tari Naliendele, Tari Serian, Tari Maruku, Tari Ukirigulu, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), taasisi ya TFRA na Tari Mlingano ambayo ndiyo maabara kuu ya utafiti wa udongo Tanzania.
Mkurugenzi wa Tari Mlingano, Mgeta Mirumba amesema kupitia programu hiyo zimekusanywa sampuli zaidi ya 100,000 kutoka ngazi ya vijiji vya mikoa mbalimbali zitakazofanyiwa utafiti na kutolea taarifa ya kiwango chake.
Ofisa Kilimo Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Ntirankiza Misibo amesema Serikali inatarajia wakulima wa vijijini watapata taarifa sahihi kuhusu kiwango cha mbolea katika mashamba yao, na kuzalisha mazao yeye kustawi kuliko kulima kwa mazoea.
