Rais Samia Awaapisha Mawaziri Wapya Na Manaibu, Makonda (Picha +Video) – Global Publishers




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa dhamana alizowapa Mawaziri na Manaibu Mawaziri wapya ni jukumu la kazi na siyo cheo cha kujivunia bila kuwahudumia wananchi.

Akizungumza leo Jumanne, Novemba 18, 2025, katika hafla ya kuwaapisha Mawaziri 27 na Manaibu Mawaziri 29 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema viongozi hao wanapaswa kuzingatia kaulimbiu ya serikali yake ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”

Amesema:

“Dhamana zetu ni dhamana za kazi na si fahari kwamba ‘na mimi ni Waziri’. Tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi. Utu uanze na sisi wenyewe viongozi.”

Rais Samia amesisitiza kuwa kuanzia sasa, kazi kubwa kwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri ni kuwajibika kwa wananchi, akibainisha kuwa ahadi kwa wananchi ni nyingi na muda wa kuzitekeleza ni mdogo. Akiweka msisitizo zaidi, amewataka baadhi ya viongozi waliokosa kasi kutokana na uzito wa miili yao “kupunguza kilo ili waendane na mwendo anaoutaka katika serikali.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipowaapisha Mawaziri wa Wizara Mbalimbali kwenye Hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma leo November 18, 2025.