Serikali kuongeza nguvu sekta ya viwanda kufikia uchumi wa dola trilioni moja

Arusha. Serikali imepanga kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za viwanda nchini kupitia uundaji wa Kanzidata ya Kitaifa ya Viwanda (NIIMS), ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kufikia uchumi wa dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.

Kwa sasa, thamani ya uchumi wa Tanzania inakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 86 mwaka 2025, na sekta ya viwanda ndiyo injini kuu ya kukua kwa uchumi huo.

Akizungumza jijini Arusha jana, Novemba 17, 2025, wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa wataalamu watakaotekeleza shughuli hiyo katika mikoa ya Manyara na Arusha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah amesema uanzishaji wa kanzidata hiyo utarahisisha utoaji wa taarifa muhimu, utengaji wa sera, upangaji wa mipango ya maendeleo na ufuatiliaji wa sekta ya viwanda.

“Katika kufikia uchumi huo tunategemea viwanda kutuinua, ndiyo maana tumeanza ukusanyaji wa taarifa za viwanda na utambuzi wa fursa za uwekezaji,” alisema.

Aidha Mpango huo unatekelezwa na TIRDO kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Ofisi ya Rais (Tamisemi).

Amesema kanzidata hiyo itasaidia kujua idadi ya viwanda vyote nchini, vikiwemo vilivyo hai, vilivyofungwa na sababu za kufungwa kwake, hatua itakayowezesha Serikali kubaini namna bora ya kufufua viwanda vilivyokufa na kuimarisha vilivyopo.

Dk Abdallah amezitaka ofisi za mikoa kushirikiana kikamilifu na TIRDO ili kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana.

Mbali na hilo amehimiza sekta binafsi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi na za kina kuhusu viwanda vyao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Madundo Mtambo, amesema mradi huo utatoa picha halisi ya uwezo wa viwanda nchini, zikiwemo taarifa za bidhaa zinazozalishwa, malighafi, masoko, ajira na changamoto wanazokumbana nazo wazalishaji.

“Taarifa hizi zitasaidia sana katika kutunga sera zinazotegemea ushahidi, kuibua fursa za uwekezaji na kuchochea ajira kwa vijana,” alisema.

Ameongeza kuwa taarifa zitakusanywa katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na zitasaidia Serikali na wawekezaji kufahamu maeneo yenye fursa kubwa na changamoto zinazohitaji kutatuliwa, ili kuimarisha sekta ya viwanda.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Mussa Massaile alisema mkoa huo una viwanda 4,006, lakini bado mahitaji ni makubwa kutokana na kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ongezeko la mahitaji ya ajira.

“Ni muhimu kujua viwanda hivi viko wapi na vinafanya nini ili kuimarisha uzalishaji na kuongeza ajira. Tuko tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kufanikisha zoezi hili,” alisema Massaile.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mariam Ahmed Haji, amesema hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuimarisha uchumi wa viwanda nchini, kuongeza uwazi wa taarifa na kurahisisha maamuzi ya Serikali na wawekezaji.

Naye mshiriki kutoka Manyara, Neema Mbise amesema Mpango huo unaweka msingi thabiti wa mageuzi ya sekta ya viwanda nchini, ikiwa ni moja ya nguzo kuu zitakazoiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa trilioni moja ndani ya miaka 25 ijayo.