Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa leo ambao unazidi kuunganishwa, mipaka ya nchi haipaswi tena kuwa ndio mwisho wa ndoto na matarajio yetu.
Kwa miaka mingi, tumekuwa tukishuhudia wanafunzi wetu wakijitahidi kumaliza masomo yao kwa lengo kuu la kutafuta kazi hapa nchini.
Ingawa hili ni jambo la msingi, mtazamo huu wa ndani unaweza kuwa kizuizi kikubwa cha fursa lukuki zilizopo nje ya mipaka yetu.
Tuna jukumu la pamoja, kama taifa, kujenga kizazi kipya cha Watanzania wenye uthubutu wa kimataifa, ambao hawatashikwa na hofu ya kuvuka bahari au anga kutafuta fursa au kuunda biashara.
Ni wakati sasa wa kuunda mfumo wa elimu ambao unawahakikishia vijana wetu kuwa raia wa ulimwengu, wenye uwezo wa kushindana na kufanya kazi popote pale.
Kwa sasa, mfumo wetu wa elimu mara nyingi huwalenga wanafunzi katika mazingira ya ndani tu. Silabasi, walimu, na hata jamii kwa ujumla, huwa na mwelekeo wa kuandaa vijana kwa soko la ajira la ndani.
Hii inawafanya wahitimu wengi kukosa ujasiri wa kutafuta fursa nje ya nchi. Wengi huamini kuwa fursa bora zaidi ziko hapa nyumbani, au hukimbia hatari ya kuanza maisha upya katika mazingira wasiyoyafahamu. Hali hii inatufanya tupoteze rasilimali muhimu ya vijana wetu, ambao wangekuwa mabalozi wa ujuzi na uzoefu wetu nje ya nchi na kurudi na utaalamu mpya wa kuendeleza nchi yetu.
Fikiria vijana wetu wanaotafuta kazi katika soko lenye ushindani mkubwa la ndani, huku kukiwa na uhitaji mkubwa wa wataalamu katika sekta mbalimbali duniani kote. Kukosa uthubutu wa kwenda mbele kunatunyima fursa ya kutumia ujuzi wetu katika ulingo mpana zaidi.
Tuutazame mfumo wetu wa elimu
Mfumo wa elimu ndio msingi wa kila kitu. Ili kufikia lengo letu, kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa katika namna tunavyowafundisha wanafunzi wetu. Kwanza kabisa, mitalaa inapaswa kupanuliwa ili kujumuisha masomo ya kimataifa.
Kufundisha wanafunzi kuhusu tamaduni mbalimbali, mifumo ya kiuchumi ya nchi nyingine, na lugha za kigeni kutawapa msingi imara wa kujiamini.
Kuanzisha programu za kubadilishana wanafunzi na nchi nyingine kutawawezesha vijana wetu kujionea hali halisi na changamoto zinazowakabili wanafunzi wenzao wa kimataifa, na hivyo kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mazingira mapya.
Zaidi ya hayo, elimu yetu inapaswa kuzingatia zaidi ukuzaji wa ujuzi muhimu wa karne ya 21 kama vile akili tunduizi, utatuaji wa matatizo, na ubunifu. Haya ni matofali ya msingi yanayowezesha mtu yeyote kufanikiwa popote pale.
Badala ya kuhimiza tu kukariri, tunapaswa kuwahamasisha wanafunzi kuuliza maswali, kufanya utafiti, na kutafuta majibu nje ya vitabu vyao. Walimu wana jukumu muhimu la kuwapa wanafunzi mifano halisi ya Watanzania waliofanikiwa nje ya nchi na kuonesha kuwa hakuna kinachowazuia wao kufanya vivyo hivyo.
Matumizi ya teknolojia, kama vile intaneti na mitandao ya kijamii, yanaweza kutumika kuunganisha wanafunzi wetu na wanafunzi wengine duniani kote na kuwafanya wawe sehemu ya jamii ya kimataifa.
Kufanya kazi au biashara nje ya nchi siyo tu suala la kupata kipato cha juu, bali pia ni suala la ukuaji wa kibinafsi na mchango kwa taifa. Fikiria mhitimu wa sekondari mwenye uthubutu wa kutaka kwenda Ghana, sio tu kwa ajili ya kutafuta ajira, bali pia kwa ajili ya kujifunza kuhusu biashara zao za kilimo au teknolojia. Au mwanafunzi anayetaka kwenda Namibia kufanya utafiti wa ikolojia ya jangwa na mbinu za uhifadhi wa wanyama. Vipi kuhusu mhitimu mwenye ndoto za kwenda Brazil kujifunza kuhusu biashara ya kahawa au mifumo yao ya nishati mbadala?
Hawa sio tu watapata ujuzi na uzoefu mpya, bali pia watarejea wakiwa na mtaji, maarifa, na mtandao mpana wa mawasiliano ambao utachangia pakubwa katika maendeleo ya nchi yetu.
Wakati mwingine, ujuzi unaohitajika nje ya nchi unaweza kuwa tofauti na ule unaopatikana hapa. Kwa mfano, mhitimu wa sekondari anaweza kuanza biashara ndogo ya kuuza bidhaa za Kitanzania nje ya nchi, na kujifunza kuhusu masoko ya kimataifa. Hili linaweza kufanyika kwa kupitia majukwaa ya biashara ya mtandaoni.
Fursa ziko nyingi, lakini zinahitaji ujasiri na maandalizi ya kutosha. Kuwa mjasiriamali wa kimataifa kunamaanisha kuwa tayari kukumbana na changamoto za tamaduni tofauti, sheria za nchi nyingine, na lugha ngeni.
Jukumu la kujenga wanafunzi wenye mtazamo wa kimataifa siyo la shule pekee. Wazazi wana jukumu la msingi la kuwakuza watoto wao kwa kuwahimiza kutafuta fursa nje ya mipaka.
Badala ya kuwaambia “kaeni karibu na nyumbani,” tunapaswa kuwahamasisha “nendeni muone dunia na mlete uzoefu hapa.”
Serikali pia ina jukumu muhimu la kurahisisha mchakato wa kusafiri kwa vijana wetu. Hii inaweza kujumuisha kutoa taarifa sahihi kuhusu fursa za masomo na ajira nje ya nchi, na hata kufanya mikataba na nchi nyingine ili kurahisisha upatikanaji wa viza na vibali vya kazi.
Sekta binafsi inaweza kuchangia kwa kutoa ufadhili wa masomo na programu za mafunzo ya kimataifa kwa wahitimu wetu bora.
Kujenga wanafunzi wa kimaataifa ni uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya taifa letu. Hatuna budi kuacha kufikiri kwa ndani na kuanza kufikiri kwa nje. Tunahitaji kuunda kizazi cha Watanzania wenye ujasiri na uthubutu, ambao wataweza kuchukua hatari, kwenda popote, na kurudi na ujuzi mpya ambao utaboresha maisha ya kila mmoja wetu.
Ni wakati sasa wa kuvunja minyororo ya mtazamo wa ndani na kufungua milango ya ulimwengu kwa vijana wetu.
