DAR ES SALAAM, Novemba 17, 2025 — Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limetoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali wanaojihusisha na utengenezaji wa mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya misitu, yakiwa na lengo la kuongeza ujuzi na kuboresha ubora wa bidhaa hiyo kufikia viwango vinavyotakiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Mhandisi Ramson Mwilangali, amesema mafunzo hayo yanajumuisha nadharia, vitendo na elimu ya uhifadhi wa mazingira pamoja na namna sahihi ya kuhifadhi bidhaa za nishati mbadala.
Wajasiriamali Kujengewa Mtandao na Kupimwa Bidhaa Bure
Mhandisi Mwilangali amesema kupitia mkutano na mafunzo hayo, TIRDO imelenga kujenga mtandao wa wajasiriamali utakaowawezesha kubadilishana ujuzi kati yao na wataalamu wa shirika hilo.
Aidha, alibainisha kuwa mara baada ya mafunzo, wajasiriamali watakaonza uzalishaji wa bidhaa hizo watapatiwa huduma ya kupimwa bure sampuli za mkaa kupitia maabara za TIRDO ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni zina ubora unaohitajika.
“Pale tutakapobaini kuna upungufu, kama taasisi tutatoa maelekezo ya nini kifanyike ili kufikia kiwango kinachotakiwa. Baada ya marekebisho, sampuli inaweza kupimwa tena na kuingia sokoni ikiwa safi na kwa gharama nafuu kwa watumiaji,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kikundi cha Fahari Kijani Group kutoka Tabora, Bw. Amiri Kassanga, amesema walipoanza kutengeneza mkaa mbadala hawakuzingatia matakwa ya viwango, lakini sasa wana matumaini makubwa ya kukuza uzalishaji kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Blamo Tech Engineering Limited, Bi. Modesta Lukosya, alisema taasisi yake imejikita katika uzalishaji wa nishati safi ili kuwaokoa wanawake na watoto ambao wamekuwa wahanga wa nishati chafu inayozalisha gesi ukaa.
“Tumejikita kwenye kuzalisha nishati safi ili kuokoa wanawake na watoto wanaoathirika na matumizi ya nishati chafu,” amesema.
Mkazi wa Mbagala, Bi. Hadija Said, ameishukuru TIRDO kwa mafunzo hayo akisema yatamsaidia kujikimu kiuchumi kama mwanamke mjasiriamali. Ameomba serikali na wadau kujitokeza kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha wahitimu kuanzisha viwanda na kuendeleza uzalishaji wa mkaa mbadala.











