Katika jamii nyingi leo, imekuwa kawaida kuona baadhi ya wanaume wakiamka asubuhi na kuondoka nyumbani wakiwa na ahadi ya kurudi jioni, lakini mara nyingi wanakimbilia kwenye vijiwe, baa au mikusanyiko ya marafiki.
Wengine hushinda huko wakipiga soga, wakicheza karata au wakijadili siasa zisizo na tija, huku familia zao zikiwa nyumbani zinasubiri ushauri, urafiki na uongozi wao.
Hawa ndio kinababa wanaoona ni “noma” au aibu kukaa nyumbani. Wanafikiri mwanaume anayekaa kwake ni dhaifu, ni mpole, au hana marafiki. Lakini huo ni upotofu mkubwa wa fikra za uanaume.
Mwanaume wa kweli ni yule anayependa nyumbani kwake. Ni yule anayepata amani, furaha na nguvu akiwa karibu na familia yake.
Kukaa nyumbani si ishara ya uvivu au upweke, ni dalili ya uwajibikaji na ukomavu wa fikra. Nyumbani ndiko panapojengwa misingi ya maadili, upendo, na uamuzi wa maendeleo. Baba akiwa jirani na familia yake, anajua kinachoendelea, anasaidia kulea watoto, anashirikiana na mama kupanga bajeti, na anajenga umoja wa kifamilia.
Lakini kinachoshangaza ni tabia ya baadhi ya wanaume wanaopendelea kutumia muda wao mwingi vijiweni. Wanajiona ni “wanaume wa mitaa” badala ya “wanaume wa nyumba.”
Kila jioni ni vijiweni, kila wikendi ni starehe, na wakati mwingine hata fedha za matumizi ya nyumbani zinaishia huko.
Hii ni ishara ya kutojitambua na kukosa dira ya maisha. Nyumba bila baba mwenye muda ni kama mashua isiyo na nahodha kwani inaweza kuelea, lakini haina mwelekeo.
Maisha ya sasa yamebadilika sana. Uchumi umekuwa mgumu, watoto wanakabiliwa na changamoto za kimaadili, na ndoa nyingi zinapitia mitihani mikubwa.
Hivyo, baba anapaswa kuwa karibu zaidi na familia yake kuliko wakati wowote ule. Wakati uliopita, labda baba angeweza kuondoka asubuhi na kurudi usiku bila matatizo, lakini dunia ya leo inahitaji uwepo wake wa kihisia na kimwili nyumbani. Watoto wanahitaji baba wa kuwasikiliza, si wa kuwasimulia hadithi za kijiweni.
Ni vizuri pia tukajifunza kutokana na matukio yaliyopita. Wakati wa vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, mbona kinababa mlikaa majumbani? Kila mmoja alikaa ndani kwa hofu ya usalama, lakini pia tuligundua kitu kimoja muhimu kwamba kwamba kukaa nyumbani ni salama, ni sehemu ya amani.
Tulikaa na familia, tukasikiliza habari pamoja, tukazungumza, na wengine hata wakapata muda wa kujitathmini. Tukio lile lilionyesha kuwa baba anaweza kabisa kuwa nyumbani bila kuona aibu, na familia ikaendelea vizuri. Swali ni: kwa nini tusifanye hivyo kila siku?
Kukaa nyumbani ni kutunza amani ya familia, ni kujenga upendo na kuimarisha mustakabali wa watoto wako. Uanaume wa kweli si kuwa maarufu mitaani, bali ni kuijenga nyumba yako iwe imara.