UDSM yamtunukia Dk Kamm shahada ya heshima ya udaktari wa fasihi

Dar es Salaam. Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mama Clementina, Dk Maria Kamm ametunukiwa shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi na Chuo Kikuu  Dar es Salaam (UDSM), kutokana na mchango wake katika kuinua elimu ya mtoto wa kike nchini.

Dk Kamm  ametunukiwa shahada hiyo ya heshima leo Novemba 18,2025 katika duru ya pili la mahafali ya 55 ya UDSM.

Anatajwa kama moja ya wanawake wachache waliofanikiwa kupata elimu wakati wa mkoloni, huku safari yake ya kufanikisha hilo ikipitia milima na mabonde.

Akisoma wasifu wake, Profesa Christine Noe kutoka UDSM amesema, Dk Kamm ni mfano wa kuigwa kama mwanamke aliyepambania ndoto zake pia kuhakikisha ndoto za elimu kwa mabinti wengine waliokata tamaa, zinatimizwa.

Akisimulia historia yake kwa ufupi amesema Dk Kamm alizaliwa Juni 1937 huko Iringa vijijini.

Amesema maisha yake ya awali yaliathiriwa na changamoto ya kukua katika jamii ambayo elimu kwa mtoto wa kike haikupewa kipaumbe kutokana na changamoto za mila na desturi kwa wakati huo.

Hata hivyo, hakukubali mila na desturi hizo zikatishe ndoto zake, kufikia mwaka 1954 alikuwa miongoni mwa wasichana tisa pekee nchini (Tanganyika wakati huo) waliofanikiwa kuhitimu kidato cha pili.

Hakuishia hapo aliendelea kusoma hadi mwaka 1957 alipohitimu masomo yake ya ualimu katika Chuo cha Ualimu Loleza.

“Tofauti na wasichana wengine ambao kwa wakati huo wengi waliishia kidato cha pili, Dk Kamm aliendelea kusoma hadi kutunukiwa shahada ya awali ya sanaa katika historia nchini Marekani mwaka 1962.

“Baadaye alijiendeleza na kutunukiwa shahada ya umahiri katika elimu mwaka 1964 nchini Marekani,  ameeleza.

Amesema hatua hiyo ilimfanya kutambuliwa kama mwanamke wa kwanza kupata shahada ya umahiri kutoka nchini Marekani.

Mchango wake katika sekta ya elimu

Profesa Noe amesema Dk Kamm pamoja na kuwa mfano katika harakati za mtoto wa kike kupambania elimu, pia amehudumu kwa muda mrefu takribani miaka 40 katika taasisi mbalimbali za elimu nchini.

Alianza safari hiyo ya uongozi katika taasisi za elimu kwa kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Machame tangu mwaka 1965 hadi 1970.

Kisha alihamia katika Shule ya Sekondari Weruweru ambayo amehudumu kama mkuu wa shule tangu mwaka 1970 hadi 1993.

“Wakati wa uongozi wake katika shule hiyo ilikuwa ya mfano katika utekelezaji wa sera ya elimu ya kunitegemea na masuala mengine ya kitaifa.

“Uongozi wake ulikuwa wa kipekee ambao ulilenga kuweka pamoja suala la malezi na nidhamu, hali iliyomfanya apendwe na wanafunzi wake hadi kumuita ‘mama’ amesema.

Mapenzi yake katika elimu ya wasichana yalimfanya kukataa fursa ya kufundisha UDSM na kuchagua kuendelea kuwafundisha na kuwalea wanafunzi wake wa Weruweru.

“Hata mwaka 1978 alipopata nafasi ya kuwa mkaguzi mkuu wa shule, alikataa nafasi hiyo na kusisitiza kuwa ameyatoa maisha yake katika kuhudumia vijana,” amesema.

Imeelezwa kuwa wakati huo aliamua kununua kiwanja na kujenga nyumba  kwa ajili ya kuwasaidia mabinti waliokuwa wakipitia changamoto mbalimbali  zinazokwamisha elimu yao, ikiwemo kupata ujauzito waliishi hapo huku wakiendelea kupata elimu na kufanya mitihani kama watahiniwa binafsi.

Miaka 35 iliyopita baada ya kustaafu alianzisha taasisi aliyoipa jina la Mama Clementina ambayo imejikita katika kuwawezesha wasichana haswa wanaotoka katika mazingira magumu kupata elimu.

“Katika kuzingatia elimu jumuishi baadaye ilianza kuwasaidia pia wavulana na hadi sasa imefanikiwa kujenga shule na vyuo vya ufundi.

“Jitihada zake zinaonyesha dhamira yake katika kuinua elimu ya mtoto wa kike, haswa wale waliotengwa kutokana na mazingira yao ili kufikia usawa na maendeleo kwa ujumla,” ameeleza.

Baada ya kutunukiwa shahada hiyo ya heshima Dk Kamm amesema, anapokea heshima hiyo kwa niaba ya wasichana wote ambao wamewahi kukata tamaa katika safari yao ya elimu na kuwatia moyo kuwa inawezekana.

“Katika maisha yangu nitaendelea kusimama mstari wa mbele katika kupigania elimu kwa mtoto wa kike na kuhakikisha wasichana wote wanapata fursa ya kupata elimu,” amesema.

Pia, ametoa wito kwa walimu na jamii kwa ujumla kuacha kunyanyapaa watoto ambao hawafanyi vizuri darasani .

Amesisitiza kuwa nao wanatakiwa kupewa fursa na kutiwa moyo ili waweze kuonyesha uwezo wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo UDSM, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar amemtaja Dk Kamm kama mtu aliyejitoa katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu.

Pia, kuimarisha elimu ya kujitegemea na kulea baadhi ya viongozi wanawake akijitolea mfano yeye binafsi akiwa mhitimu aliyefundishwa naye.

Akitoa nasaha zake kwa wahitimu balozi Mwanaidi amesema mahafali hayo siyo mwisho wa safari yao ya kitaaluma bali ni mwanzo wa safari mpya iliyojawa na fursa, majukumu na nafasi ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“Wahitimu shahada yenu ni wito wa kutumikia kwa maarifa, maadili, na ujasiri wa kuleta mabadiliko. Nendeni mkasimamie haki, ubunifu na uadilifu popote mnapokwenda,” amesema.

Naye Mlau katika mahafali hayo, Profesa Agnes Mwakaje, amewataka wahitimu wanaporudi kwa jamii wakadhihirishe taaluma zao kwa vitendo na kuwa chachu ya mabadiliko chanya.

Pia, amewasisitiza kumtanguliza Mungu katika kila wanachokifanya kuwa wasikivu na wanyenyekevu.

“Msichoke kuwa na upendo kwa kila mtu bila kujali jinsi, uwezo, dini au rangi maana wema ni hazina, Pia dunia ina mambo mengi chagua ya kukujenga achana na yanayokuharibu hata kama yanavutia sana.

“Zaidi sana nawaasa mkautumie ujuzi mlioupata kwa umahiri na kwa kuzingatia maadili ya fani mlizozisomea,” amesema.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye amesema katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji chuo kimeendelea na mapitio, uhakiki, uidhinishaji na maombi ya ithibati ya mitaala katika programu mbalimbali.

Amesema zaidi ya mitaala 250 imepitiwa na inatarajiwa kuwasilishwa kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) kwa ajili ya kupitishwa.

Ameeleza kuwa hadi sasa mitaala 49 imepata ithibati kwa mwaka 2025/2026.

Amesema takribani asilimia 40 ya programu zilizopitishwa zinatolewa kwa njia mseto (blended learning) ikionyesha mwelekeo mpya wa ufundishaji unaochanganya mtandaoni na ana kwa ana.