Usalama ziwani: Vyombo visajiliwe, vitambulisho vitumike

Geita. Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Chato, Avodia Sylivester, amesema juhudi za kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu tahadhari za kiusalama wanapokuwa ziwani zimechangia kupunguza vifo ambavyo hapo awali vilikuwa vikiripotiwa katika Ziwa Victoria.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya sekta hiyo, jana Jumatatu Novemba 17, 2025 Sylivester amebainisha kuwa tangu kuimarishwa kwa kampeni za utoaji elimu, hakuna kisa hata kimoja cha mvuvi kufariki dunia majini kilichoripotiwa mwaka huu, jambo analolitaja kama hatua kubwa ya mafanikio katika kulinda uhai wa wavuvi na kuimarisha ustawi wa jamii.

Ofisa Uvuvi Wilaya ya Chato,Avodia Sylvester akitoa elimu kwa wavuvi wilayani Chato.

Sylivester amefafanua kuwa miaka ya nyuma hali ilikuwa tofauti, kwani licha ya uwepo wa idadi kubwa ya mitumbwi, uelewa wa wavuvi kuhusu masuala ya usalama ulikuwa mdogo, jambo lililochangia vifo kati ya 20 hadi 30 kwa mwaka kutokana na ajali ziwani.

Amesema vifo hivyo mara nyingi vilihusishwa na kukumbwa na dhoruba, kuzama kwa vyombo vya uvuvi au wavuvi kutozingatia kanuni za usalama.

Sylivester amesema hali hiyo sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa, kutokana na elimu endelevu inayotolewa na idara ya uvuvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

“Taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa hutumwa kwa wakati, na wavuvi wengi wamekuwa wakizipokea moja kwa moja kupitia simu zao. Hii imewasaidia kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuelekea ziwani.

Godfrey Chegere,Ofisa Mfawishi kutoka Wakala wa Meli (Tasac) mkoani Geita, akizungumza na wavuvi katika Mwalo wa Chato Beach wilayani Chato.

“Endapo kuna taarifa ya upepo mkali, mawimbi makubwa au hatari yoyote, ujumbe hutolewa mapema, na wavuvi wamekuwa wakitii maagizo hayo kwa kutoingia ziwani hadi hali itakapokuwa salama,” amesema.

Pia, Sylivester amewakumbusha wavuvi kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapopokea wageni wasiowafahamu, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na vitendo vya unyang’anyi vinavyoweza kufanywa na watu kutoka maeneo mengine.

Aniset Magayane, ambaye ni mvuvi, anabainisha kuwa mara nyingi wavuvi wamekuwa wakinusurika na mawimbi makali ziwani kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Magayane amesema hali hiyo imekuwa changamoto kubwa hasa kwa wavuvi wenye kipato cha chini, na hivyo anaomba Serikali kuwasaidia ili waweze kujikinga ipasavyo wanapofanya shughuli zao.

“Gharama za vifaa vya usalama ni kubwa na wengi wetu hatuwezi kumudu, ndiyo maana mara nyingi tunamtegemea Mungu atulinde.

“Katika mitumbwi zaidi ya 200 iliyopo hapa, ukitafuta wavuvi wenye ‘life jackets’ utakuta ni wachache, kwa sababu bei yake ni ya juu.

“Mara nyingi unakuta mtumbwi unaondoka na watu wanne au watano, lakini mmoja tu ndiye anayekuwa na ‘life jacket’. Ikitokea ajali, wengine wanakuwa hatarini, ingawa kwa rehema za Mungu bado hatujawahi kupata ajali mbaya,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Chato Louis Bura.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Louis Bura, amewakumbusha wavuvi kuhakikisha wanasajili vyombo vyao wanapotekeleza shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria, akisema hatua hiyo itarahisisha utoaji wa msaada wa dharura endapo watakumbana na majanga wakiwa ziwani.

Bura ameeleza kuwa utaratibu wa usajili ni muhimu kwa kuwa unawawezesha wavuvi kutambuana kirahisi, ikizingatiwa Mwalo wa Chato Beach huwahusisha wavuvi kutoka maeneo mbalimbali, wakiwemo wanaotoka Muleba.

Ameongeza kuwa usajili huo utarahisisha pia ukaguzi wa vyombo ili kubaini kama vinakidhi vigezo na vinafaa kutumika katika shughuli za uvuvi.

‘’Wananchi wetu kila wanapotembea wawe na vitambulisho vinavyotambulika kitaifa, tuna kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpigakura kinakubalika na kwa watumishi vitambulisho vyao vya kazini vinatambulika, lakini pia paspoti za kusafiria na kwa wale ambao hawana kitambulisho kabisa, tuna viongozi wetu wa vitongoji na vijiji, wanaweza kufika pale wakapewa barua ya utambulisho yenye muhuri,” amesema.

Bura amesema hayo wakati akifungua semina ya tahadhari kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Victoria kupitia mwalo wa Chato Beach iliyoongozwa na Wakala wa Meli nchini (Tasac).

‘’Wananchi msajili vyombo vyenu ni kwa manufaa yenu wenyewe, lakini vilevile ni kwa maendeleo ya nchi yetu, Serikali inajali hali ya usalama ya wananchi ili linapotokea jambo lolote, tujue chombo kile kilielekea mwelekeo upi, na tunapotafuta tujue chombo hiki kilisajiliwa wapi, lakini pia inawezesha kufahamu kama chombo hicho kinafaa kuingia ziwani,” amesema.