Vurugu za Oktoba 29: Samia aonyesha mashaka Tanzania kupata mikopo kimataifa

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonyesha wasiwasi wa kuwepo uwezekano wa Tanzania kukumbwa na ugumu wa kupata mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa, kutokana na matukio ya siku ya uchaguzi.

Amesema matukio hayo, yameitia doa Tanzania na huenda yakasababisha ipate changamoto ya kupata mikopo hiyo, huku akiwaelekeza watendaji wake kujikita katika matumizi ya rasilimali za ndani kutekeleza miradi iliyopangwa.

Sambamba na hilo, ameahidi kuendelea na utaratibu wa kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, kila atakapobaini baadhi ya wateule wake wanatumia nafasi walizopewa kama fahari, badala ya dhamana kwa wananchi.

Oktoba 29 na 30, mwaka huu kulitokea maandamano yaliyozaa vurugu zilizosababisha kuuawa kwa raia, kuharibiwa kwa mali za watu binafsi na miundombinu ya umma.

Hatua hiyo, imezisababisha jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), kutoa wito wa kutafutwa njia za kudumisha amani nchini, huku Jumuiya ya Madola ikituma ujumbe wa mazungumzo ya maridhiano.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Novemba 18, 2025 alipozungumza baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

“Yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo, kwa hiyo huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza wa awamu hii,” amesema.

Katika muhula wake wa kwanza, amesema Tanzania ilipata mikopo mingi kwa sifa, msimamo na kazi zake, lakini kwa doa lililopo sasa huenda hali ikawa tofauti.

Kutokana na mazingira hayo, amesema ni jukumu lake na viongozi aliowateuwa kuhakikisha wanafanya kazi ya kutafuta fedha za ndani kupitia rasilimali zilizopo ili kutekeleza miradi inayotarajiwa.

“Muhula wa pili wa awamu ya sita, tutaanza kufanya miradi wenyewe alafu mashirika yatatukuta njiani tutakwenda nao. Hatutakaa kusubiri, tunauza mradi, tunakwenda kubembeleza, mradi unakubaliwa, lakini nendeni karekebisheni hili, nenda kamkisi usimnyukue.

“Mradi badala ya kupata uidhinishaji miezi mitatu minne, tunachukua mwaka mzima tunabembeleza mradi mmoja, hadi ruhusa inatoka tuna miaka miwili tunamaliza kipindi chetu, hatutasubiri hayo, tutaanza na watatukuta katikati,” amesema.

Katika hotuba hiyo, ametangaza kwamba hataona shida kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, iwapo kutakuwepo na wateule watakaozitumia nafasi walizopewa kama fahari badala ya dhamana ya kuwatumikia wananchi.

“Mimi sioni shida kubadilisha na mnanijua na kipindi fulani mlinisema kuwa nabadilisha sana. Na nilisema nabadilisha mpaka nipate yule atakayefanya kazi na mimi kwa moyo mmoja,” amesema.

Amewataka wahakikishe wanawajibika kwa wananchi na Taifa, hasa ukizingatia kuna muda mchache wa kwenda mbio kutekeleza yaliyoahidiwa.

“Aliye mzito akapunguze kilo kidogo tuna kazi ya kwenda mbio na ni mbio hasa kwa sababu muda mchache, mambo ni mengi,” amesema.

Amesema nafasi za uteuzi ni kupishana, ndiyo maana baadhi ya waliokuwepo hawapo sasa na kuna sura mpya zilizochanganyika na chache za zamani.

Lakini, amesema hata waliokuwepo walifanya kazi nzuri na matokeo yanayoshuhudiwa sasa ni matokeo ya juhudi za bidi zao.

“Lakini kazi hizi ni kupishana. Kwa hiyo wamepishana. Kuna timu mpya na kongwe imechanganyika ili twende tukaendeleze mapambano ya maendeleo kwa wananchi,” amesema.

Rais Samia amewaambia wateule hao kuwa, kiapo maana yake wamekubali kubeba majukumu na anaamini wameyabeba kwa moyo mkubwa na kwamba wako tayari kwenda kuwatumikia watu.

“Majukumu tuliyopeana leo ni dhamana sio fahari, kwamba na mimi ni Waziri ikawa ndio fahari, ulikotoka unakokaa na kwingineko hapana. Tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi,” amesema.

Ameeleza kwa kuwa kauli mbiu ni Kazi na Utu, tunasonga mbele, utu huo unapaswa kuanza na viongozi hao, kisha kuwaonyesha kwa watu wengine na kuuheshimisha.