WADAI 100 KUONGEZWA KWENYE HATI YA MASHTAKA YA DKT. MANGURUWE


UPANDE wa Mashtaka katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vanilla International, Simon Mkondya maarufu Dkt. Manguruwe, umedai kuwa unatarajia kusoma hoja za awali Novemba 20, mwaka huu.
Wakili wa serikali Titus Aaron amedai hayo leo Novemba 18, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki.
Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kuomba muda wa nyongeza kufuatia kubaini kuwepo kwa wadai wengine zaidi ya 100 ambao ni sehemu ya ushahidi na wanapaswa kuongezwa kwenye hati ya mashtaka.
Shauri hilo lenye namba 31523/2024 lilipangwa kutajwa leo kwa ajili ya kusomwa hoja za awali, lakini shughuli hiyo iliahirishwa baada ya Jamhuri kueleza kuwa kumekuwa na walalamikaji zaidi ya 100 ambao hawakuingizwa kwenye hati ya mashtaka.
Wakili Aaron amedai kuwa maelezo ya walalamikaji hao ni sehemu ya rekodi ya shauri na wanatarajiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa, hivyo hawatakiwi kuingizwa kwenye hati baada ya ushahidi kuanza kusikilizwa.
Amedai kuwa hatua inayofuata ni kuongeza idadi ya wadai pekee kwani upelelezi umeshakamilika.
Upande wa utetezi ulipinga hoja hiyo ukidai kuwa shauri limefikishwa mahakamani tangu Novemba 5, 2024, na kwa kipindi chote hicho Jamhuri ilikuwa ikisema upelelezi haujakamilika.
Hata hivyo, wiki iliyopita walieleza kuwa upelelezi umekamilika na kuwapatia nyaraka kama taratibu zinavyoelekeza.

Utetezi ulidai kuwa kuongezwa kwa wadai hao sasa ni ishara kuwa upelelezi bado haujakamilika, hivyo wakaomba shauri liendelee kama ilivyopangwa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Nyaki aliiahirisha kesi hadi Alhamisi, Novemba 20, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali na kuuagiza upande wa Jamhuri kuhakikisha umeweka taarifa za nyongeza katika hati ya mashtaka.
Mbali na Dk Manguruwe, mshtakiwa mwingine ni aliyekuwa mkaguzi wa kampuni hiyo, Rweyemamu John kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kujipatia zaidi ya Sh milioni 90 kwa kununua viwanja tisa katika eneo la Idunda, Mkoa wa Njombe.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, makosa hayo yanadaiwa kutendwa kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam. Washtakiwa wanadaiwa kufanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kupata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizoweka na kujipatia Sh milioni 92.2 kutoka kwa watu 19.
Inadaiwa kuwa kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 1, 2023, Dkt. Manguruwe alijipatia viwanja tisa katika eneo la Idunda mkoani Njombe akijua kuwa vinatokana na makosa ya upatu. Mshtakiwa John yuko nje kwa dhamana, huku Dkt. Manguruwe akiendelea kushikiliwa mahabusu kutokana na shtaka la utakatishaji fedha.