Dar es Salaam. Wadau wa kada mbalimbali nchini Tanzania wamekuwa na maoni mbalimbali juu ya tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza uvunjifu wa amani uliotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 wakisema muundo wake na aliyeiteuwa inafanya ikose kuaminiwa.
Kauli hizo za wadau zinazotoka na hatua ya Rais Samia kuunda tume hiyo yenye wajumbe saba itakuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande.
Wajumbe ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya.
Katika tume hiyo, pia yumo Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi David Kapya na Waziri mstaafu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa kile alichoahidi Novemba 14, mwaka huu alipohutubia Bunge la 13, akisema amehuzunishwa na matukio hayo na kwamba ataunda tume kuchunguza.
Katika matukio hayo, baadhi ya watu wamepoteza maisha, kujeruhiwa wengine wamepoteza mali na miundombinu ya umma imeharibiwa na kuchomwa moto.
Miongoni mwa maoni ya wadau wanahoji tume hiyo iliyoundwa kukosa viongozi wa dini na au asasi za kiraia ambao wangeweza kuifanya kuaminika zaidi kwa wananchi na hata ripoti yake pindi itakapokamilika.
Wadau hao wametoa mitizamo hiyo walipozungumza na Mwananchi pamoja na kupitia mitandaoni kujionea jinsi wanavyoizungumzia.
@Franklinrosa yeye amehoji uwepo wa Jaji Joseph Warioba na viongozi wa dini huku Gerald Cmd Mahita yeye anasema: “Tume bila viongozi wa dini.” Hoja hiyo imeulizwa na jackson marwa akisema: “Nilitegemea viongonzi Wa dini wawemo.”
@Mkimbizimweusi, alishauri kuongeza kwa viongozi wa dini katika orodha hiyo.
Naye, Ngoda 507 ameendika uteuzi umezingatia weledi hivyo, walioteuliwa wakamsaidie Rais Samia. Ameongeza Rais Samia amewaamini hivyo wakachape kazi.
Naye Mchambuzi wa Siasa, Said Majjid amesema itakuwa na matokeo iwapo ingeundwa na mtu ambaye si sehemu ya wanaodaiwa kuwa sababu ya tukio hilo.
Amesema Rais Samia anatajwa kuwa miongoni mwa upande unaotuhumiwa hakupaswa kuiunda tume hiyo, kwa sababu haitaaminika.
Mbali na hilo, amesema hata walioteuliwa kuiongoza tume hiyo wapo miongoni mwa wateule wake katika nyakati mbalimbali hivyo unakosakana uhakika kwamba wanaweza kueleza ukweli iwapo itabainika Mkuu wa nchi ana makosa.
“Kunahitajika tume huru. Tunaposema tume huru tunamaanisha tume inayoundwa na mamlaka huru na mtu asiyekuwa sehemu ya upande unaolalamikiwa,” amesema.
Amesema muundo wa tume hiyo, ulipaswa kuhusisha wajumbe ambao wote ni majaji na vema zaidi ingehusisha watu kutoka nje ya Tanzania.
“Kwa sababu kwa vyovyote wajumbe hawa hawataaminika kwa sababu wameteuliwa na mamlaka ambayo pia itachunguzwa. Muhimu ni kuaminika na wananchi,” amesema.
Kwa upande wa Mchambuzi wa Utawala, Dk Lazaro Swai amesema kuundwa kwa tume ni jambo jema lakini, yatengenezwe mazingira yatakayofanya iaminiwe.
Amesema kuaminiwa kwa tume hiyo, kutatokana na uhuru wake ambao kwanza unaanzia kwa wajumbe ilionao hadi muundo wake na inaripoti kwa nani.
“Kama nia ni maridhiano baadaye basi tume inapaswa iundwe na iwe na eneo la kuripoti na sio kuripoti kwa Mkuu wa nchi ambaye naye kuna watu wanamhusisha na tuhuma,” amesema.
Ameeleza kwa namna ilivyo, tume hiyo itapata kigugumizi linapokuja suala la kueleza ukweli unaomhusu aliyeiteuwa. Pengine hautawekwa hadharani au hautaelezwa kabisa.
Amesisitiza ni muhimu kuwe na mazingira yanayoaminika na watu wengi ili kuanza uchunguzi.
Mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke amesema ni hatua nzuri kuundwa kwa Tume hiyo, akisema Rais Samia ametekeleza kile alichokiahidi katika siku za hivi karibuni.
“Sijajua hadidu za rejea au mwongozo watakaopewa katika utekelezaji wa majukumu yao, lakini Tume imesheheni watu wazoefu naamini watakuja kitu kizuri,”
“Ni watu wenye uzoefu mzuri, tunamaani watakuja na taarifa nzuri kama watapewa mwongozo wa kufanya kazi yao. Ni hatua nzuri ya kuunda Tume na wajumbe wapo vizuri,” amesema Dk Kyauke.
