Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya shule,lengo likiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Alisema mpango huo unajumuisha ujenzi wa shule mpya za awali, msingi na sekondari, pamoja na madarasa mapya katika shule zilizopo.
“Tunapaswa kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kutosha ya kusoma, bila kuteseka kutokana na msongamano wa madarasa. Serikali imejipanga kuwekeza katika shule mpya na ujenzi wa madarasa mapya katika shule zilizopo ili kila mwanafunzi asome kwa uhuru na usalama.” alisema na kuongeza:
“Hii ni jitihada ya kuhakikisha tunaweka misingi thabiti ya elimu bora, si kwa sasa tu bali kwa vizazi vijavyo. Hatuwezi kusalia nyuma, lazima tuweke mazingira yanayofaa kwa watoto wetu.”
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu hapa nchini wameipongeza hatua hiyo ya Serikali na kusema kazi kubwa sasa ni utekelezaji.
Akizungumza na Mwananchi, mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie, amekiri umuhimu wa hatua hiyo.
“Tayari kazi na nguvu kubwa imekwishafanyika kwenye eneo hili, kwahiyo ile kutamka jana ni msisitizo unaokwenda kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa elimu yetu. Kauli ya Rais anapohutubia Bunge ni kama mpango wa kufanyiwa kazi; ametoa maelekezo kwa Bunge na watendaji wa serikali yake,” alisema.
Dk Loisulie alisema kuwa licha ya uwezekano wa changamoto mpya kutokana na ongezeko la idadi ya watu, mpango huo ni jitihada ya dhati ya kupunguza msongamano.
“Hatuwezi kusema tutafika mahala ambapo hatutahitaji madarasa mapya, lakini nia ya Rais Samia ni kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira mazuri yaliyoboreshwa,” ameeleza.
Kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Afisa Elimu Sekondari, Dk Mussa Ali, amethibitisha utekelezaji wa mpango huo.
“Tumejizatiti kuanza majengo ya ghorofa za kisasa zitakazopunguza msongamano wa wanafunzi. Hivi sasa tuna ghorofa nane zikiwa kwenye hatua za mwisho za ujenzi. Moja kati ya hizo imegharimu kiasi cha Sh 2.2 bilioni na kila moja lina madarasa 20 pamoja na matundu 45 ya vyoo.
“Aidha, kwa watoto wenye mahitaji maalum, tunajumuisha lift. Shule zingine mbili ziko Kitunda na Upanga Magharibi, zikiwa na madarasa ya Tehama, maabara za sayansi na mifumo ya intaneti” alisema Dk Ali.
Katika hotuba yake Rais Samia aliweka bayana umuhimu wa usimamizi bora wa miradi ya elimu: “Hatua hii itafanikiwa tu ikiwa kila mmoja atahakikisha uwajibikaji. Haiwezekani kujenga madarasa na kuacha usimamizi” alisema.
Pamoja na mpango huo mkubwa, walimu na wazazi wanatarajia matokeo chanya. Mwalimu wa shule moja ya Serikali, ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema:
“Kusema kweli, darasa langu la kidato cha pili lina wanafunzi 478. Ni idadi kubwa kuliko uwezo wa kawaida wa kufundisha. Tatizo la msongamano linaathiri ufundishaji kwa kiasi kikubwa; mwalimu hawezi kumfikia kila mwanafunzi”
“Tumepokea hotuba ya rais kwa matumaini makubwa. Madarasa mapya yatawezesha ufaulu bora na nidhamu rahisi kusimamia.” alisema.
Mzazi mwingine aliyezungumza na Mwananchi na kujitambulisha kwa jina la Grory Jonathan mkazi wa Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam alieleza furaha yake na mpango huo:
“Nimezipokea taarifa hizi kwa shauku. Binti yangu yupo kidato cha lwanza na darasa lake lina zaidi ya wanafunzi 360. Wakati mwingine anarudi nyumbani akilalamika kuwa haoni ubao vizuri. Natarajia maboresho haya yatasaidia watoto kupata umakini zaidi na kuongeza ufaulu.”
Mzazi mwingine wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Mohammed Salum, alisisitiza kuwa msongamano unaathiri ubora wa elimu:
“Wanafunzi 350–400 darasani ni changamoto kubwa. Mwalimu hawezi kufundisha kwa ufasaha na nidhamu inakuwa ngumu kusimamia. Mpango huu wa Serikali ni hatua nzuri, lakini tunataka utekelezaji uwe wa haraka na uwe na ufuatiliaji wa karibu. Zaidi ya madarasa, ningependa kuona vyoo vya kutosha, mabweni, maabara za kisasa na madawati vinapelekwa shuleni.”
Wazazi na walimu kwa ujumla wanakubaliana kuwa mpango huu wa rais Samia ni kielelezo cha dhati cha dhamira ya Serikali kuhakikisha mapya katika shule zilizopo ili kila mwanafunzi asome kwa uhuru na usalama.
