Dar es Salaam. Katika baraza jipya la mawaziri, miongoni mwa teuzi zilizowakosha Watanzania wengi wa maeneo mbalimbali ni wa Dk Dorothy Gwajima, waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Tabia ya kuvaa uhalisia, kuwa mfuatiliaji wa mambo hususan mitandaoni, kujibu na kusimamia hoja huku akiongoza kwa kubebesha watu wajibu wao, vimetajwa kuwa kete za kiongozi huyo.
Novemba 17, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa mawaziri na manaibu 56 watakaohudumu katika Wizara 27 kwa maana mawaziri 27 na naibu 29. Katika mgawanyo huo wanaume ni 77 na wanawake asilimia 23 akiwemo Dk Dorothy Gwajima anayeshika nafasi hiyo kwa kipindi kingine.
Katika zama za mitandao ya kijamii, Waziri Gwajima ameweka kambi huko, akijenga hoja na ushawishi kupitia majukwaa ya dijitali, na kuibuka kama mfano wa uongozi unaojibu haraka sauti za wananchi.
Gwajima, ameibuka kama mmoja wa viongozi wanaotumia kwa kasi mitandao ya kijamii kujenga uhusiano wa karibu na wananchi. Uwepo wake mtandaoni umekuwa chanzo cha kujibu changamoto za jamii, lakini pia umefungua mlango wa mjadala mpana kuhusu uongozi wake.
Kupitia akaunti zake za Instagram na X (zamani Twitter), Dk Gwajima ameunda daraja hai kati ya Serikali na wananchi, akijihusisha moja kwa moja na maoni, malalamiko na mapendekezo ya wananchi.
“Anajua kuuvaa uhalisia, anafuatilia, anajibu, anasimamia, anaongoza na anabebesha watu wajibu wao. Anaishi na sisi, ni miongoni mwetu kwa hiyo anaaminiwa na Watanzania wengi,” anamwelezea Saldin Kimangale, mtaalamu wa saikolojia, alipozungumza na Mwananchi.
Vyombo vya uchunguzi wa hali ya kijamii vinaonyesha maelfu ya raia hutuma ujumbe wao wa matatizo ya kijamii na kikatiba kupitia mitandao, na mara nyingi waziri anajibu moja kwa moja, akionyesha uwajibikaji wa kisiasa na kijamii.
Njia hii ya mawasiliano ya haraka na ya uwazi imeelezea kile ambacho wachambuzi wa ndani wanasema ni maboresho ya uwajibikaji wa Serikali na uhusiano wa moja kwa moja na raia badala ya kuwa tu matangazo ya sera.
Dk Gwajima amekuwa akitoa onyo kali kwa waandaaji wa maudhui (content creators) mitandaoni, akitaka wasitoe maudhui yanayodhalilisha, yanayochochea ukatili wa kijinsia au yanayokiuka sheria na miongozo ya maadili.
Kwa upande mwingine, anaunga mkono mapambano ya msingi ya kijamii pia anahamasisha kuondoa matumizi ya simu kwa watoto, akitaka wadau wa teknolojia na mawasiliano kujadili vikwazo vya usalama wa watoto kwenye mitandao.
Dk Gwajima anaelezwa kama kielelezo cha Serikali ya kijamii inavyoweza kuendeshwa katika enzi ya mitandao. Kiongozi anayesikiliza, anayejibu, na kuingilia kati mjadala kwa vitendo.
“Ameifanya mitandao kama ofisi ya pili ya waziri, amejijengea taswira ya kiongozi anayefuatilia hoja za wananchi kwa karibu.
Ujumbe mbalimbali wa wananchi kuhusu ukatili wa kijinsia, malezi ya watoto, pamoja na changamoto za huduma za kijamii sisi tunauwasilisha kupitia mitandao, na mara kadhaa waziri hujibu papo hapo,” amesema Henry Haule, mmoja wa wafuasi wa Dk Gwajima kwenye mtandao wa Instagram.
“Nilikuwa nasali sana Mama (Samia, Suluhu Hassan) asikosee kabisa katika hii wizara na asitubadilishie waziri kabisa, sasa safi hongera mama (Gwajima) kwa mara nyingine tena hakika Mungu aendelee kukupigania hivi hivi,” ameandika mmoja wa wafuasi wake mtandaoni.
“Safi, nafasi hiyo anaiweza, nategemea kukuona Arusha Tengeru Maendeleo ya Jamii kwenye graduation (mahafali) ,” ameandika Reymasha5.
Licha ya sifa anazopata, mitandao hiyohiyo imekuwa pia uwanja wa wakosoaji wake.
Baadhi ya watumiaji mitandaoni wamehoji kama uwapo wake mkubwa mtandaoni ni sehemu ya kuongeza uwazi au ni taswira inayofunika changamoto za kiutendaji katika ngazi za chini.
Wapo wanaosema maagizo anayoyatoa kwa maofisa wa maendeleo ya jamii ikiwamo kusimamia majukwaa ya uwezeshaji wanawake vijijini, yanawaongezea mzigo bila kuelezwa rasilimali wanazopaswa kutumia.
Wengine wamekuwa wakitaka kuona mizani ya maneno na matokeo katika maeneo ya ukatili wa kijinsia, mkazo wa sera, pamoja na huduma za watoto wenye mahitaji maalumu.
Wachambuzi wa masuala ya utawala wanasema mtindo huo umempa Dk Gwajima nafasi ya kipekee kuonekana miongoni mwa viongozi wanaoifikisha Serikali moja kwa moja kwa wananchi.
Ni wazi kwamba uhusiano wake na mitandao si tu maonyesho ya kisiasa, bali sehemu ya mabadiliko makubwa ya jinsi viongozi wa Tanzania wanavyowajibika kwa wananchi wao.
Akimwelezea zaidi, Mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduku amesema mbali na ushawishi wake mtandaoni, Dk Gwajima ameendelea kujitambulisha kupitia misimamo yake mikali dhidi ya maudhui hatarishi mitandaoni, ikiwamo video zinazodhalilisha watoto au kueneza ukatili wa kijinsia.
“Ametoa maagizo kwa waandaaji wa maudhui kujikita katika maadili, hatua ambayo imeungwa mkono na sehemu ya jamii inayohofia ongezeko la maudhui yenye athari kwa watoto na vijana.
“Vilevile, amekuwa mstari wa mbele kusisitiza malezi bora, makuzi ya awali ya mtoto na juhudi za kupunguza ukatili maeneo ambayo wizara yake imekuwa ikitoa taarifa za kupungua kwa baadhi ya matukio,” amesema Nduku.
Kwa jicho la kijamii, Dk Gwajima amejijenga kama waziri anayechagua kusimama katikati ya majukwaa ya dijitali na yasiyo ya dijitali. Hata hivyo, umaarufu huu pia unamweka kwenye mizani ya umma kila siku.
Wananchi wanabaki na maswali: Je, kasi yake ya kuwajibika mitandaoni inaleta mabadiliko ya vitendo kijijini na mtaani?
Je, misimamo yake kuhusu maadili mitandaoni inaweka msingi wa sera jumuishi au inaathiri uhuru wa ubunifu? Na je, uhusiano wake wa karibu na wananchi unaweza kubeba uwezo wa kubadilisha mifumo ya kijamii ambayo imekuwa ikipigiwa kelele kwa miaka mingi?
Kwa sasa, Dk Dorothy Gwajima anabaki kuwa miongoni mwa viongozi wanaovutia mjadala mkubwa nchini, mchanganyiko wa ushawishi wa kidijitali, sauti thabiti kuhusu malezi na maadili, na changamoto za uongozi katika wizara yenye majukumu makubwa ya kijamii.
Kwa kadiri mitandao inavyozidi kuwa sehemu ya maamuzi ya kisiasa na kijamii, ndivyo jina lake litakavyoendelea kuzungumziwa kwa pongezi, kwa ukosoaji na kwa matumaini ya mageuzi ya kweli.
