Baba wa kijana aliyeuawa Israel asimulia alivyokosa usingizi kwa miaka miwili

Hai. Wakati Serikali ikikabidhi mabaki ya mwili wa Joshua Mollel (21) aliyeuawa kwenye mapigano ya Israel na Palestina, baba mzazi wa kijana huyo, Loitu Mollel amesimulia namna alivyokosa usingizi kwa miaka miwili akisubiri kupatikana kwa mwili wa mwanaye.

Mabaki ya mwili huo yamewasili leo   Novemba 19, 2025 na kupokewa na viongozi wa Serikali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Balozi Silima Haji Kombo, wazazi, ndugu pamoja na marafiki katika Uwanja wa ndege wa  Kimataifa wa Kilimanjaro, KIA.

Joshua ambaye alikuwa miongoni mwa vijana 260 wa Kitanzania waliokwenda nchini Israel kwa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo  alitekwa na kuuawa Oktoba 7,2023 wakati akifanya mazoezi ya kilimo Kusini mwa Israel, wakati  wapiganaji wa Hamas walipowavamia na mwili wake kuchukuliwa na wapiganaji hao.

Katika mapigano hayo Clemence Mtenga, mkazi wa Wilaya ya Rombo aliuawa na kurejeshwa nchini wakiwa na raia wengine wa mataifa mbalimbali waliotekwa katika mapigano hayo kwenye eneo la Gaza.

Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akiwakabidhi wazazi wa kijana Joshua Mollel (21) Shada la Maua mara baada ya mabaki ya  mwili wake kuwasili katika Uwanja wa ndege wa  Kimataifa wa Kilimanjaro, KIA.Picha na Janeth

Baba mzazi wa Joshua afunguka

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kupokea mwili huo, Mzee Mollel amesema miaka miwili tangu apate taarifa za kuuawa kwa mwanaye alishindwa kupata usingizi.

“Nimefika hapa kupokea mwili  wa mwanangu kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho, miaka yote miwili sikuwa na amani lakini kwa sasa namshukuru Mungu kwa sababu mwili umepatikana na tukishauhifadhi basi maisha mengine yataendelea,” amesema Mzee Mollel.

Mzee Mollel  amesema, mwanaye Joshua alikuwa ni mtiifu, mtaratibu ambaye hana makuu na kwamba watamkumbuka daima.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Israel na Tanzania kwa kipindi chote ambacho ilimuonyesha ushirikiano wa hali na mali na kuhakikisha mwili wa mwanaye umepatikana.

Jeneza lenye mabaki ya mwili wa kijana Joshua Mollel ( 21) anayedaiwa kuuawa kwenye mapigano ya Israel na Palestina likiwa katika  Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) ulipowasili nchini  Novemba 19, 2025. Picha na Janeth Joseph

“Kutoka moyoni, nashukuru Serikali ya Israel kwa jitihada tangu haya yalipotokea Oktoba 7, 2023,  tangu kipindi hicho hawakuwahi kukata mawasiliano na sisi na hata mwili ulipopatikana,” amesema Mzee Mollel.

Amesema; “Sina budi kushukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje, kila wakati wa kipindi chote ambacho wamekuwa wakiwasiliana na sisi hadi kuwezesha kupatikana kwa mabaki ya mwili wa mwanangu.”

Aidha, amesema kesho Oktoba 20 wanatarajia kuzika mabaki ya mwili wa kijana huyo, mtaa wa Njiro, kata ya Orkesumet, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mabaki ya mwili wa  Joshua,  Balozi Musa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na familia mpaka hatua za mwisho.

Mama na baba mzazi wa kijana Joshua Mollel ( 21) anayedaiwa kuuawa kwenye mapigano ya Israel na Palestina wakiwa wamebeba shada la maua, mara baada ya kupokea mabaki ya mwili wa kijana wao katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, KIA.Picha na Janeth Joseph

“Serikali kupitia ubalozi wake mjini Tel Aviv ilifuatilia upatikanaji wa mabaki ya mwili wa marehemu, na vipimo vya kisayansi vilifanyika (DNA)  na kuthibitisha kama huu ni mwili wa mwenzetu Joshua Mollel,” amesema Balozi Musa.

Amesema; “Serikali tangu kipindi hicho imefuatilia mpaka kupatikana kwake Novemba 6, 2025, tuliarifiwa na kupata ithibati kwamba ni mwili wa mtoto wetu  Mollel na leo tuko hapa kupokea mabaki ya mwili wake, kwa ajili ya mazishi ya kesho kijijini kwao Simanjiro.”

Aidha, amesema Serikali ina mchango wake mkubwa katikati kufanikisha mazishi hayo kwa kila linalowezekana pamoja na kufanikisha mazishi  Joshua.

Mwakilishi wa Ubalozi wa Israel nchini Kenya ambaye ameiwakilisha Tanzania, Nonga Lewenstein akiweka shada la maua kwenye jeneza lenye mabaki ya  mwili wa Joshua Mollel (21) aliyeuawa nchini Israel Oktoba 7, 2023.Picha na Janeth Joseph

“Tumepata faraja kubwa ya mashirikiano ambayo tumeyapata kwa serikali ya Wilaya ya Simanjiro, tuendelee kumwombea dua Mwenyezi Mungu amuweke kwenye waja wake  wema peponi amina, tutaendelea na mashirikiano katika mazishi na kupeana faraja,” amesema Balozi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro,  Fakii Lulandana amesema Watanzania wanapaswa kupata somo la uzuri wa amani, kwani mapigano ndiyo yamesababisha kifo hicho.

Lulandana amesema Watanzania wamezoea kuishi kwa uhuru na amani, hivyo wanapaswa kuendelea kuienzi amani kwani ni tunu ya Taifa.

Aidha, ametoa  pole kwa familia ya marehemu Joshua, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo mara baada ya kuwasili kwa mabaki ya mwili huo.

“Kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga anatoa pole na watashiriki pamoja katika maziko yatakayofanyika kitongoji cha Njiro Mji mdogo wa Orkesumet,” amesema.