Njombe. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, ametoa onyo na tahadhari kwa madereva wa bajaji na bodaboda mkoani humo, akiwataka kuwakataa watu watakaofika mkoani humo ili kuwashawishi kufanya vurugu na uvunjifu wa amani wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika yanayotarajiwa kufanyika Desemba 9, mwaka huu.
Kamanda Banga ametoa onyo hilo leo, Novemba 19, 2025, alipokuwa akizungumza na baadhi ya madereva wa bajaji na bodaboda katika ofisi za chama chao zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Amesema kuwa Oktoba 29, 2025 kulifanyika uchaguzi mkuu nchini, na katika Mkoa wa Njombe hakukujitokeza vurugu yoyote.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuendeleza hali hiyo ya amani kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, hasa ikizingatiwa kuwa mkoa huo ni miongoni mwa mikoa yenye shughuli nyingi za kibiashara.
“Ukiona gari la polisi siku hiyo linapita ujue halipo kwa ajili yako bali kwa wale waliokuja kuwachochea kufanya vurugu na naomba watu wakija kuwachochea ili mfanye vurugu muwakatae,” amesema Banga.
Amewataka madereva hao kutoa taarifa mapema endapo wataona viashiria vya mtu yoyote kushawishi wananchi kufanya vurugu ili waweze kumuhoji aliyemtuma kufanya hivyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Madereva wa Bodaboda Wilaya ya Njombe, Velmund Msigwa, amesema kuwa madereva wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa utulivu, na kwamba yeyote atakayehusika katika maandamano au kusababisha uvunjifu wa amani atakuwa amepoteza sifa ya kuendelea kufanya kazi ndani ya mkoa huo.
“Mwanachama yoyote atakayepatikana na kosa la kuvunja amani ya Tanzania hatakuwa na sifa ya kuendesha pikipiki mkoa wa Njombe,” amesema Msigwa.
Mmoja ya madereva wa bodaboda, Onesmo Ng’ang’ama amesema suala la amani ni muhimu ili kuendelea kujitafutia kipato huku wakidai kuwa kilichotokea Oktoba 29,2025 kiliwaweka kwenye wakati mgumu kwa kuwa wengi wao wanafanya kazi kwenye pikipiki za mikataba.
“Maandamano yanapojitokeza kuna shughuli zinasemama kipindi kile tulisimama kufanya kazi kutokana na machafuko yaliyotokea mikoa jirani hivyo ilituathiri sana,” amesema Ng’ang’ama.
