BOT YAWAPIGA MSASA WAANDISHI WA HABARI KUTOKA MIKOA MITANO

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kusisitiza majukumu yake ya msingi katika kulinda uthabiti wa uchumi wa nchi kwa kuboresha mifumo ya malipo, kusimamia taasisi za kifedha na kuhakikisha mazingira salama kwa wananchi katika shughuli zao za kifedha.

Aidha, imehimiza wananchi kujenga utamaduni wa kutunza fedha na kuwa na matumizi bora ili kupunguza uwepo wa fedha chafu, hatua itakayosaidia kuepusha gharama kubwa za kuchapisha upya fedha.

Meneja Msaidizi wa Uchumi kutoka BoT, Tawi la Dodoma, Shamy Chamicha, alisema hayo Novemba 19, 2025 wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Benki Kuu na sera mpya ya fedha, katika semina inayowakutanisha waandishi wa habari kutoka Dodoma, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar inayoendelea jijini Dodoma.

Chamicha alibainisha kuwa jukumu kubwa la BoT ni kuandaa, kuchapisha na kutekeleza Sera ya Fedha sambamba na kusimamia mzunguko wa fedha nchini, kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki katika kiwango tulivu.

“Kupitia sera za fedha, benki hufanya tathmini ya mara kwa mara kuhusu mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki kudhibiti ongezeko au upungufu wa fedha kwenye mzunguko,” alieleza.

Aidha, aliongeza kuwa BoT inasimamia kwa karibu taasisi za kibenki na zisizo za kibenki ili kuhakikisha zinafuata sheria, kanuni na taratibu za kuzuia utakatishaji fedha, hatua inayolenga kulinda wateja na kuhakikisha huduma za kifedha zinatolewa kwa usalama na weledi.

Chamicha alifafanua pia, BoT ina jukumu la kusimamia akiba ya fedha za kigeni, kuimarisha thamani ya sarafu ya Tanzania na kutoa sarafu mpya pale inapohitajika ili kukidhi mahitaji ya mzunguko wa fedha katika uchumi.

Awali akifungua semina hiyo, Meneja wa Idara ya Uendeshaji wa BoT, Tawi la Dodoma, Nolasco Maluli, alisema mafunzo hayo yataleta uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya fedha na uchumi, jambo litakalowawezesha kuandika makala, taarifa na takwimu sahihi kuhusu sera za fedha na mifumo ya malipo.

Maluli alisisitiza, BoT inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya uchumi, masoko ya fedha na usimamizi wa mifumo ya malipo.

Alitaja baadhi ya mada zinazojadiliwa katika mafunzo hayo kuwa ni muundo na majukumu ya BoT, Sera ya Fedha Inayotumia Riba, elimu kuhusu hati fungani, elimu ya fedha na usajili wa vikundi, ulinzi na huduma za kifedha na usimamizi wa mifumo ya malipo na alama za usalama katika noti za Tanzania.