Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewatahadharisha wateule wa Rais Samia Suluhu Hassan kwamba wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na viwango vinginevyo wategemee kuchukuliwa hatua.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 19,2015 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kihongosi amesema waziri ama naibu waziri ambaye hatatimiza wajibu wake kwa viwango na akasababisha kumuangusha Rais Samia hawatamvumilia.
Hata hivyo, Rais Samia jana Novemba 18, 2025 alipowaapisha mawaziri 27 na manaibu waziri 29, aliwaonya kuhusu uwajibikaji akisema hatasita kubadilisha viongozi hao kila itakapobidi hadi atakapopata anayemfaa.
Kihongosi amesema chama kinatarajia utendaji wa kiwango cha juu kutoka kwa viongozi walioteuliwa, akibainisha wengi wao ni wapya na wanapaswa kufahamu Rais hana mchezo katika kushughulikia masuala ya utendaji serikalini.
“Chama hakitasita kuchukua hatua kali kwa kiongozi yeyote atakayekuwa mzembe, wajue wana wajibu wa kuwatumikia Watanzania ili kutimiza ndoto za mkuu wa nchi,” amesema Kihongosi.
Kihongosi amesema hatua ya Rais Samia kuomba mamlaka husika kuwaachilia huru baadhi ya vijana waliokuwa wakishikiliwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni, hivyo chama kinatarajia Serikali kusimamia ipasavyo ahadi hizo.
Ametaka wateuliwa wote wakafanye kazi na watendaji wa Serikali wahakikishe utekelezaji wa ahadi ya siku 100 uje na matokeo.
Aidha, ameonya chama kitawachukulia hatua watendaji wote watakaoshindwa kutimiza wajibu wao au kuendeleza vitendo vya rushwa, akisema kuwa upimaji wa utendaji utafanyika na watakaobainika watawajibishwa mara moja.
Katika hatua nyingine, Kihongosi alimpongeza Rais Samia kwa kuunda tume ya uchunguzi kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika matukio hayo, vurugu zilitokea mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Geita, Arusha, Mara na Ruvuma na kusababisha raia kuuawa, wengine kujeruhiwa huku mali za watu binafsi na miundombinu ya umma vikiharibiwa.
Tume hiyo yenye wajumbe saba inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Wajumbe walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya.
Katika tume hiyo, pia yumo Balozi Paul Meela, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi David Kapya na Waziri mstaafu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax.
Pia, Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza kuwa kurejesha amani inapopotea ni kazi kubwa na yenye gharama kwa taifa.
