Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji akiwataka wawekezaji wa ndani kujitokeza kujenga miradi mikubwa, inayoacha alama badala ya kuwa watazamaji.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Novemba 19, 2025 wakati akizindua mradi wa Hoteli ya Tembo Kiwengwa Beach Resort Zanzibar, amesema atapenda kuona miradi mikubwa ya uwekezaji hususani katika sekta ya utalii ikiwa ya wazawa.
“Ninapenda kuona wazawa wengi wakishiriki kuwekeza miradi, sipendi kuona miradi mikubwa hapa inakuwa na wawekezaji wageni, naomba sisi tusiwe watazamaji bali tushiriki, na sisi tutaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
“Naomba wazawa wengine wafuate nyayo za mwekezaji huyu ili tukifika mwaka 2030 tuache miradi yenye alama na nimefurahi sana maana tunaposema tuache alama ndio hizi za wazawa kushiriki kwenye miradi mikubwa,” amesema Dk Mwinyi akimpongeza mwekezaji huyo mzawa.
Kiongozi huyo amesema wawekezaji kama hao wanaisaidia Serikali katika mipango yake ya kutoa ajira 350,000 maana inakuwa ni sehemu ya kuzifikia ajira hizo.
Mbali na ajira, pia hoteli hiyo itasaidia wajasiriamali na wavuvi kwani watakuwa wakiuza bidhaa zao katika hoteli hiyo.
Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi na mwekezaji Hussein Ibrahim Muzamill wakifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa hoteli ya Tembo Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Tunaposema utalii kwa wote ndio huu, kila mmoja ananufaika kupitia miradi hii, ajira zinapatikana kwa vijana Wetu, wajasiriamali wetu wanauza bidhaa zao kwenye hizi hoteli,” amesema Dk Mwinyi.
Ameeleza namna ambavyo azima yao ya kufikisha watalii milioni moja kwa mwaka inakwenda kufikiwa akisema katika mwezi uliopita watalii walifikia 704,300.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema mradi huo una thamani ya Dola za Marekani 12 milioni sawa na Sh29 bilioni.
Amesema ndani ya kipindi cha miaka mitano tayari Zipa imesajili miradi 550 ikiwa na thamani ya Dola za Marekani 6.5 bilioni sawa na Sh15.7 trilioni ambayo itatoa ajira 25,000.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2025 pekee, Zipa imesajili miradi 135 yenye thamani ya Dola za Marekani 700 milioni sawa na Sh1.6 trilioni.
“Hii imepindukia ikilinganishwa na uwekezaji kwa mwaka na mara hii miradi mikubwa ipo kisiwani Pemba,” amesema Saleh.
Kuhusu mradi huo pekee, Saleh amesema umegharimu Dola za Marekani 12 milioni.
Naye Mwekezaji wa mradi huo, Hussein Ibrahim Muzamill amesema Serikali inawathamini wawekezaji hususani wazawa.
Kwa mujibu wa Yasser, mradi huo utatoa ajira kwa wazawa kati ya 150 hadi 200.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zahro Mattar amesema miradi kama hiyo inasaidia kuongeza ajira na kuinua kipato cha mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla.
Mattar amesema katika mkoa huo kuna hoteli na nyumba za kulala wageni 375 zinazotoa ajira 9,000, ukiwa unachukua asilimia 35 ya miradi yote ya utalii iliyopo Zanzibar.
“Hata hivyo, tumekuwa na changamoto kidogo ya usalama kwa wageni, lakini tayari tumeshaanza kuyashughulikia kwa kukaa na wadau mbalimbali kuangalia namna ya kudhibiti,” amesema.
Naye Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema watatekeleza mipango yote kuhakikisha uwekezaji unazidi kukua kila mara.
“Tunaomba mwekezaji afikirie kwenda kuwekeza miradi kama hii kisiwani Pemba maana mazingira yameboreshwa,” amesema.
