Fahamu maana ya ‘Accept Cookies’ unapoingia katika tovuti kwa mara ya kwanza

Dar es Salaam. Je, unafahamu unapoingia katika tovuti kisha ukabofya ‘Accept Cookies’ unakuwa umekubali nini?

Mara nyingi unapotembelea tovuti kwa mara ya kwanza, basi utakutana na ujumbe unaosema “Accept cookies”. Kwa lugha rahisi, hii ni ruhusa ambayo tovuti inaomba ili iweze kuhifadhi taarifa zake ndogo kwenye simu au kifaa chako ulichotumia kingia.

Cookies ni mafaili madogo yanayotengenezwa na tovuti unazotembelea. Zinatumika kuhifadhi taarifa za matumizi yako mtandaoni na kusaidia kufanya uperuzi wako uwe rahisi zaidi.

Faili za Cookies pia hutumiwa na tovuti husika kukukumbuka, kuboresha huduma na wakati mwingine kuonesha matangazo yanayokufaa.

Kwa mfano, tovuti zinaweza, kukusaidia kuingia bila ya kuandika upya nywila (Password), kukumbuka mipangilio yako ya ukurasa husika (Settings), pia kukupa taarifa zinazokuhusu au zenye uhusiano na eneo ulipo.

Cookies zinaweza: kukumbuka jina ulilotumia kuingia (login), kuhifadhi lugha unayopendelea kutumia, kuhifadhi bidhaa ulizoweka kwenye sehemu ya ununuzi mtandaoni pamoja na kuwezesha tovuti kupima idadi ya watembeleaji.

Kuna aina mbili za Cookie

Kwanza kuna First-party cookies ambazo hutengenezwa na tovuti unayotembelea moja kwa moja (inayoonekana kwenye anwani ya juu). Pia, kuna Third-party cookies ambazo hutengenezwa na tovuti nyingine ambazo zimepachikwa ndani ya tovuti unayotumia, kwa mfano: matangazo, picha au video kutoka huduma za nje.

Hizi mara nyingi hutumika kutoa matangazo yanayokulenga au kukufuatilia kwenye tovuti mbalimbali.

Hata hivyo, si lazima ukubali. Ukikataa (“Reject” au “Decline cookies”), baadhi ya huduma kwenye tovuti zinaweza kutofanya kazi ipasavyo, hasa zile zinazotegemea kukukumbuka kama mtumiaji.

Kwa ujumla, cookies hutolewa katika makundi mbalimbali kama vile; necessary cookies zinazohitajika kuendesha tovuti, analytics cookies zinazofuatilia takwimu za matumizi, advertising cookies zinazolenga kukuonyesha matangazo kulingana na tabia zako za mtandaoni.

Kwa hiyo, unapokutana na “Accept cookies”, unakuwa unaamua kama tovuti hiyo ikukumbuke au la, kulingana na faragha unayoitaka.

Kwa nini unahitajika kukubali cookies?

Kisheria, tovuti haziruhusiwi kuendesha cookies bila kukupa taarifa na kupata ridhaa yako wewe kama mtumiaji.

Ikumbukwe Sheria ya ePrivacy Directive (Cookie Law) inahitaji: wamiliki wa tovuti kuwaeleza watumiaji kuwa wanaendesha cookies, pia kuzizuia cookies zinazo hitaji ridhaa hadi mtumiaji atakapokubali pamoja na kuonyesha cookie banner zinapofunguliwa tovuti.

Jinsi ya kufuta, kuruhusu au kusimamia Cookies kwenye Browser ya Chrome.

Unapotumia Google Chrome, unaweza kufuta cookies zilizopo, kuruhusu au kuzuia cookies, na kuweka mipangilio maalumu kwa tovuti fulani.

Kama ukitaka kufuta cookies basi unapaswa ujue kwamba ukizifuta, unaweza kutoka kwenye akaunti zako moja kwa moja (logout) na mipangilio ya tovuti inaweza kufutika.

1.    Fungua Chrome kwenye kompyuta.

2.    Nenda juu kulia, bofya More (alama ya nukta tatu).

3.    Chagua Delete browsing data.

4.    Chagua kati ya Basic au Advanced, halafu chagua Cookies and other site data.

5.    Kwenye sehemu ya “Time range”, chagua muda unaotaka kufuta:

o     Muda wote (All time)

6.    Chagua data nyingine unazotaka kufuta.

7.    Bofya delete data ili kudhibitisha.

Jinsi ya kufuta cookies za tovuti fulani tu

2.    Bofya More (nukta tatu juu kulia), kisha Settings.

3.    Nenda Privacy and security → Third-party cookies.

4.    Bofya See all site data and permissions.

5.    Tumia sehemu ya juu kulia kutafuta jina la tovuti.

6.    Kwenye upande wa kulia wa jina la tovuti, bofya delete.

7.    Thibitisha kwa kubofya delete tena.