Hakimi, Mayele, Mzize walivyong’ara Tuzo za CAF 2025

Beki na nahodha wa timu ya taifa ya Morocco na klabu ya PSG, Achraf Hakimi, ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka Afrika katika hafla ya utoaji wa tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) zilizofanyika leo Jumatano Novemba 19, 2025 huko Rabat, Morocco.

Hakimi amewashinda Mohamed Salah wa Misri na klabu ya Liverpool na mshindi wa tuzo hiyo mwaka 2023, Mnigeria, Victor Osimhen anayecheza Galatasaray.

Wakati Hakimi akiibuka kinara wa wanaume, Mmorocco mwingine, Chebbak anayecheza klabu ya Al-Hilal Ghizlaine, pia ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika kwa Wanawake.

Hakimi katika msimu wa 2024-2025, aliiongoza PSG kutwaa mataji matatu makubwa, sambamba na uongozi wake ndani ya Timu ya Taifa ya Morocco iliyofuzu Kombe la Dunia 2026 na wenyeji wa AFCON 2025.

“Katika anga lililojaa nyota, kuna inayong’aa kupita zote! Yeye. Ni yeye tu. Hakimi. Mchezaji Bora wa Mwaka!,” limefafanua chapisho lililowekwa na CAF katika akaunti zaks rasmi za mitandao ya kijamii.

Akiwa na PSG, Hakimi amesaidia kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2024-2025 kwa mara ya kwanza. Pia alikuwa Mmorocco wa kwanza na Mwafrika wa saba kufunga bao katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akifanya hivyo katika fainali wakati PSG ikiichapa Inter Milan mabao 5-0, huku yeye akifunga la kwanza. Mataji mengine ni Ligi Kuu ya Ufaransa na Coupe de France, akikamilisha treble ya msimu.

Katika msimu wa 2024-2025 kwenye mashindano yote, alifunga mabao 8 na kutoa asisti 12.

Kuanzia Januari hadi Oktoba 2025, aliongeza mabao 9 na asisti 11 kwa PSG na timu ya taifa ya Morocco kwa pamoja.

Kwa upande wa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Klabu, tuzo imekwenda kwa Fiston Mayele, mshambuliaji wa Pyramids na taifa la DR Congo.

Mayele amemshinda mchezaji mwenzake wa Pyramids, Mohamed Chibi raia wa Morocco ambaye ni beki wa kulia. Mwingine ni mshambuliaji wa RS Berkane na timu ya taifa ya Morocco, Oussama Lamlioui.

Tuzo ya Bao Bora la Mwaka 2025 imebebwa na mshambuliaji wa Yanga na Taifa Stars, Clement Mzize.

Mzize ameshinda tuzo hiyo kutokana na bao alilofunga msimu wa 2024-2025 hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe wakati Yanga ikishinda 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam,  Januari 4, 2025.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mzize alikuwa anashindana na wenzake 12 lakini kura zilizopigwa na mashabiki, zimempa ushindi huo.

Kwa upande mwingine, kipa wa Nigeria na Brighton, Chiamaka Nnadozie ameshinda tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka wa Wanawake kwa mara ya tatu mfululizo katika Tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) 2025. Amewashinda Andile Dlamini kutoka Afrika Kusini na Khadija Er-Rmichi wa Morocco.

Mchezaji Bora Wanaume – Achraf Hakimi (Morocco / Paris Saint-Germain)

Golikipa Bora Wanaume – Yassine Bounou (Morocco / Al Hilal)

Mchezaji Bora wa Klabu Wanaume – Fiston Mayele (Pyramids/ DR Congo)

Kocha Bora Wanaume – Bubista (Cape Verde)

Mchezaji Bora Chipukizi Wanaume – Othmane Maamma (Morocco / Watford)

Timu Bora ya Taifa Wanaume – Morocco U20

Klabu Bora ya Wanaume – Pyramids FC

Mchezaji Bora Wanawake – Ghizlaine Chebbak (Morocco / Al Hilal)

Golikipa Bora Wanawake – Chiamaka Nnadozie (Nigeria / Brighton & Hove Albion) –

Mchezaji Bora Chipukizi wa Kike – Doha El Madani (Morocco / AS FAR)

Timu Bora ya Taifa Wanawake – Nigeria