Wito huo umetolewa leo Novemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa ITA anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Dkt. Emmanuel Masalu wakati alipokutana na wanachuo waliohitimu, wafanyakazi na wadau mbalimbali wa sekta ya kodi, ikiwa ni maandalizi ya mahafali ya 21 yanayotarajiwa kufanyika Novemba 21,mwaka huu.
Dkt. Masalu amesema ajenda ya maendeleo duniani imehama kutoka Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwenda katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo yanasisitiza zaidi umuhimu wa kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa rasilimali za ndani.
Amebainisha kuwa kipindi cha MDGs, nchi nyingi ziliitegemea sana misaada ya nje na ufadhili wa wafadhili katika kutekeleza miradi yao ya maendeleo.
“Mwito wa kuchochea ukusanyaji wa rasilimali za ndani ni mkubwa kuliko wakati mwingine wowote. Ni wakati wa nchi kutumia kikamilifu vyanzo vyake vya mapato na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje,” alisema.
Amesisitiza kuwa ajenda ya SDGs inahimiza mataifa kuongeza uwezo wao wa kukusanya mapato ya ndani, jambo linalofanya ‘mobilization’ya rasilimali za ndani kuwa kipaumbele muhimu kwa maendeleo endelevu.
Pia, Dkt. Masalu ameeleza kuwa mahafali hayo ni jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa, mawazo na ubunifu miongoni mwa wanafunzi, wahitimu na wadau wa sekta ya kodi.
Kwa upande wake, Judith Frugence muhitimu wa chuo hicho mwaka 2010 ambaye ana kampuni yake ya masuala ya kodi ambaye pia ni Msimamizi katika Kampuni ya Cynophei Consultants, alishiriki safari yake binafsi ya ujasiriamali, akionyesha umuhimu wa kupata uzoefu wa moja kwa moja wa kazi kabla ya kuanzisha biashara.
Amesema hapo awali alikusudia kuingia kwenye ushauri elekezi (consultancy), lakini aligundua haraka kuwa alihitaji kuimarisha ujuzi na kupata fursa za kuyatumia katika mazingira halisi ya kazi.
Frugence alihamia Mwanza ambako alikabiliana na changamoto mpya pamoja na fursa katika mji ambao hakuwa ameuzoea.
“Mwaka wangu wa kwanza ulikuwa mgumu, lakini mitandao niliyoijenga na kuthubutu ilimfungulia milango aliyokuwa hajawahi kuifikiria na ili kuharakisha maendeleo yangu nilijitolea kufanya kazi kwa miezi sita, nikiboresha ujuzi wangu wa Excel na uwasilishaji,”anasema
Anasema uzoefu huo ulimsaidia kupata nafasi baadaye katika Citibenk, ambako alipata uzoefu wa moja kwa moja kwenye mifumo mikubwa na ya kisasa ya kifedha.
Anasema hatimaye alijiunga na taasisi nyingine iliyooana zaidi na malengo yake ya ujasiriamali. Kila hatua ilimfundisha mbinu za usimamizi wa rasilimali, kujenga mahusiano na kufikiri kimkakati, na hivyo kumjengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kibiashara kama mjasiriamali aliyekomaa.
Kwa upande wake, Karimu Chitundu, Rais wa Baraza la Wanafunzi ITA, amesema anatarajia ujumbe wa mahafali hayo utachochea wanafunzi kujiamini na kuingia kwenye ajira binafsi.
Amesisitiza kuwa kwa elimu na ujuzi wanaopata ITA, wahitimu wana uwezo wa kujitengenezea fursa na kufanikiwa kupitia ujasiriamali.
Ameongeza kuwa wanafunzi pia wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika kampuni za ushauri elekezi, wakitumia utaalamu wao kujenga taaluma zenye mafanikio na zenye mchango kwa jamii.

