Jeshi la Zimamoto na Uokoaji latangaza nafasi za ajira

Dar es Salaam. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini limetangaza nafasi mpya za ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 19, 2025, ajira hizo zinawalenga vijana wenye sifa za kuanzia elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita, stashahada hadi shahada.

Taarifa hiyo imesainiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John  Masunga, ni kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Sura ya 427 na Kanuni za Utumishi za mwaka 2008. 

Taarifa hiyo imeleza waombaji wa elimu ya kidato ncha nne wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, wenye afya njema, bila kumbukumbu za uhalifu, wasiokuwa wameoa au kuolewa, na wenye umri wa miaka 18 hadi 25.

Masharti mengine ni kutokuwa na alama za kuchora mwilini, kutotumia dawa za kulevya, na kuwa tayari kuhudhuria mafunzo ya taaluma ya Zimamoto na Uokoaji. 

Taarifa hiyo imeweka wazi kuwa ngazi ya kidato cha nne na sita,   nafasi zilizotangazwa zinahusu madereva wa magari makubwa, wauguzi, wataalamu wa Zimamoto na Uokoaji, matabibu, mafundi mchundo wa magari, wazamiaji na waogeleaji, wanamichezo, wanamuziki wa brass band, waandishi waendesha ofisi, wataalamu wa Tehama na mafundi umeme wa ndege.

Aidha,  waombaji wote hao wanatakiwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 28, huku madereva wakihitajika kuwa na leseni daraja E na watafanyiwa uhakiki wa vitendo. 

Kwa ngazi ya shahada, nafasi zimetolewa kwa wahandisi bahari, wahandisi wa Tehama, wahandisi wa ndege, wakadiriaji majenzi (QS), wataalamu wa sheria waliomaliza shule ya sheria kwa vitendo, wahandisi mafuta na gesi, wahandisi ujenzi, mitambo na umeme.

Waombaji wa nafasi hizo nao wanatakiwa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 28 na sifa zote za msingi.

Taarifa hiyo inaelekeza kuwa maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kupitia mfumo wa ajira wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia tovuti ya  https://ajira.zimamoto.go.tz kabla ya Desemba 03, 2025.

Aidha, waombaji wanatakiwa kuambatisha barua ya maombi iliyoandikwa kwa mkono, fomu ya uthibitisho wa afya kutoka kwa mganga wa Serikali, nakala ya kitambulisho cha Taifa (Nida), namba za mitihani ya kidato cha nne na sita, vyeti vya taaluma vinavyotambulika na serikali, pamoja na barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji/Mtaa.

Jeshi hilo limeeleza kuwa barua zitakazowasilishwa kwa njia ya posta, mkono au barua pepe hazitapokelewa.

Aidha, imesisitizwa kuwa nakala za vyeti vingine lazima ziwe zimeidhinishwa na kamishna wa viapo au hakimu na  waombaji wote wanatakiwa kuandika namba za simu kwenye barua zao za maombi.

Jeshi limetoa onyo kuwa yeyote atakayewasilisha nyaraka za kughushi au taarifa za uongo atachukuliwa hatua za kisheria.