KLABU ya Yanga, leo Jumatano Novemba 19, 2025 imezindua jezi maalum kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025-2026, huku zikizua gumzo mtandaoni kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa soka, baadhi yao wakionyesha kutofurahishwa nazo.
Yanga imepangwa kundi B la michuano hiyo na timu za Al Ahly ya Misri, JS Kabylie (Algeria) na AS FAR (Morocco) ambapo mechi ya kwanza itachezwa Jumamosi wiki hii Novemba 22, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, saa 10:00 jioni.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema uzinduzi wa jezi hizo walipanga kuufanya kesho Alhamisi Novemba 20, 2025, lakini wamelazimika iwe leo kwa sababu ya kupokea maoni kutoka kwa mashabiki kuhitaji haraka.
Yanga wamezitambulisha jezi hizo kupitia akaunti zao rasmi za mitandao ya kijamii ambapo kuna ya nyumbani yenye rangi ya kijani, ugenini rangi ya njano na ile ya tatu yenye rangi nyeusi.
Muda mfupi baada ya kutambulishwa kwa jezi hizo, wadau mbalimbali wametoa maoni akiwemo Taimuly Hussein24, kupitia Instagram, alikomenti chapisho lililowekwa na Yanga akisema: “Tafuteni mbunifu mwingine, hapa hamna mbunifu, hovyo kabisa.”
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Arushafunnyboy, amekomenti: “Mimi ni mwana Yanga ila hizi hapana aiseee😂😂😂😂 nachoka Baba yenu.”
Khalifa khalid Abdallah, naye amekomenti: “Mwaka huu tutanunua ila mmetushusha viwango😢😢😢😢.”
Vitenge-original-quality, amekomenti: “Jezi kama jeneza😂😂.”
Sharobaro-wa-instagram-tz, amekomenti: “Timu yangu lakini wacha niseme moyoni, mwakani hebu nipeni na mimi hiyo kazi ya kutengeneza jezi jamani, naona ya njano kuna ngao, hivyo ni bora mnipe tu mimi kwa sababu mmeshashiba ubwabwa tayari.”
Msabaha-msabizness, amekomenti: “Uzi uko poa ila tafadhali yule Sheria Ngowi tubonge nae kwa sababu ana jicho sana kwenye kutengeneza.”
‘Nduttum1’, amekomenti: “Ni ngumu sana kuitetea Yanga🙌🙌.”
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la ‘Emma The Boy’, amekomenti: “Is sheria Ngowi still alive? We need him kwa kweli😂😂😂😂, akimaanisha ni “Kweli bado Sheria Ngowi yupo hai? Tunamuhitaji yeye kwa kweli.”
Sophy_canavaro23 naye amekomenti katika jezi za rangi ya kijani kwamba: “Ila Yanga Jaman!! Mnataka tukaibe 😂😂 Hali ni ngumu Uzi mkali🙌🙌”
“Afadhali ata ya huu kidogo ntauvaa😢 izo zingine ni madekio,” amekomenti alvan.s.c.o.t katika chapisho la jezi nyeusi.
Katika jezi hizo, kwa mujibu wa komenti nyingi za wadau, nyeusi ndiyo imekubalika zaidi, ikifuatiwa na ya kijani, kisha ya njano.